Mali, Senegal, Somalia, Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimelaani shambulio baya la kigaidi lililotokea siku ya Jumatano kwenye kituo cha tasnia ya ulinzi katika mji mkuu wa Uturuki.
"Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inalaani vikali shambulio la kigaidi lililotokea Ankara. Tuko pamoja na familia za wahasiriwa, na tunawatakia afueni ya haraka waliojeruhiwa,” ilisema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje.
"DRC inathibitisha tena mshikamano wake na Uturuki na kujitolea kwake kwa uthabiti katika mapambano dhidi ya ugaidi wa aina zake zote," iliongeza.
Hapo awali, rais wa serikali ya mpito ya Mali, Kanali Assimi Goita, pia alilaani shambulio hilo.
"Tunalaani vikali shambulio la kigaidi kwenye makao makuu ya kampuni ya anga ya Uturuki mjini Ankara," Goita alisema katika taarifa.
'Tuko Pamoja'
Akielezea "mshikamano kamili" na Uturuki, "mshirika wa kimkakati wa Mali katika suala la ulinzi," alisema yuko pamoja katika wakati huu mgumu na familia za wahasiriwa.
Takriban watu watano waliuawa na 22 kujeruhiwa wakati magaidi waliposhambulia majengo ya Kiwanda cha Anga cha Uturuki (TAI) kulingana na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya.
Magaidi hao "walikatwa makali," aliongeza.
Mkuu wa Baraza la Utawala wa Mpito la Sudan na Mkuu wa Vikosi vya Wanajeshi, Luteni Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan pia alituma salamu za rambirambi kwa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na watu wa Uturuki.
"Nawatakia, kwa niaba ya watu na serikali ya Sudan, salamu zangu za rambirambi kwa wahasiriwa wa shambulio la kigaidi, ambalo lilisababisha vifo na majeruhi kadhaa," Al-Burhan alisema katika taarifa yake.
Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye alitaja shambulio hilo kuwa la "uoga."
"Ninalaani vikali shambulio la kigaidi la Uturuki. Ni kitendo cha woga na cha kinyama. Kwa niaba ya watu wa Senegal, ninatoa salamu zangu za rambiranbi na tuko pamoja na Rais wa Uturuki (Recep Tayyip) Erdogan, familia za wahasiriwa na Watu wa Uturuki wenye urafiki," Faye alisema.
"Tunawatakia rehema za Mungu kwa waliouawa na afueni ya haraka kwa waliojeruhiwa."
'Kitendo cha uoga'
Wakati huo huo Somalia ililaani tukio hilo, na kulitaja kuwa ni shambulio la kigaidi " baya".
"Kitendo hiki cha woga sio tu shambulio dhidi ya Uturuki, lakini ni tishio kwa amani na usalama duniani. Somalia, ikiwa imekabiliwa na changamoto kama hizo, iko pamoja na Uturuki," Wizara ya Mambo ya Nje ilisema katika taarifa.
Somalia inapongeza mwitikio wa haraka wa vikosi vya usalama na ina imani kwamba waliohusika watafikishwa mahakamani, taarifa hiyo ilisema.
Mogadishu inatoa rambirambi zake kwa familia zilizoathirika na kusema inasimama kwa pamoja na watu na serikali ya Uturuki.
"Somalia inasimama pamoja na Uturuki na jumuiya ya kimataifa katika mapambano dhidi ya ugaidi, kwa ushirikiano unaozingatia maadili ya pamoja na kuaminiana," ilisema, na kuitaka jumuiya ya kimataifa "kuimarisha ushirikiano dhidi ya ugaidi."
"Kwa pamoja, tunaweza kuhakikisha kuwa vitendo kama hivyo havidhoofishi azma yetu ya kulinda watu wetu na kudumisha amani," ilisema.