Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema kuwa msimamo wa haki wa nchi yake kuhusu Gaza utathibitishwa na historia kama ilivyokuwa nchini Syria.
"Kama vile tulivyothibitishwa kuwa na msimamo wa haki nchini Syria, historia pia itathibitisha haki yetu katika mgogoro wa Gaza," Erdogan alisema katika hafla ya Kundi la Wauzaji Bidhaa za Uturuki nje huko Istanbul siku ya Ijumaa.
Assad, kiongozi wa Syria kwa takriban miaka 25, alikimbilia Urusi baada ya makundi yanayopinga utawala kuchukua udhibiti wa Damascus mnamo Desemba 8, na kumaliza utawala wa Chama cha Baath, ambacho kilikuwa madarakani tangu 1963.
Erdogan pia alisisitiza kuwa Uturuki ndiyo nchi pekee ambayo imesitisha kabisa biashara na Israeli.
Mwezi Mei, Uturuki ilisitisha muamala wote wa kibiashara na Israeli ambayo ni sawa na kiwango cha dola bilioni 9.5, huku kukiwa na vita vinavyoendelea vya mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza.
Licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka kusitishwa kwa mapigano mara moja, jeshi la Israeli limeendeleza vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza ambavyo vimesababisha vifo vya takriban wahanga 45,600 wengi wao wakiwa wanawake na watoto tangu Oktoba 7, 2023.
Israeli imeweka vizuizi vya kulemaza huko Gaza, na kuwaacha wakazi wake, haswa wakaazi wa kaskazini mwa Gaza, kwenye hatihati ya njaa.
Uturuki imekuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Israeli tangu kuanza kwa kampeni ya kijeshi na imetoa msaada mkubwa wa kibinadamu kwa Gaza, ikiwa ni pamoja na chakula, vifaa vya matibabu, na kuwahamisha maelfu ya wagonjwa.