Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametoa wito wa umoja baina ya mataifa ya Kiislamu ulimwenguni kuwaunga mkono Wapalestina na Walebanoni dhidi ya manyanyaso kutoka kwa Waisraeli.
Katika risala yake aliyoitoa wakati wa mkutano wa 40 wa Kamati ya Kudumu ya Uchumi na Ushirikiano wa Kibiashara wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (COMCEC) jijini Istanbul siku ya Jumatatu, Erdogan alisisitizia hali ya kibinadamu inayoendelea katika eneo la Gaza, akiiita ni kuwa ni "moja ya mauaji ya kinyama zaidi katika karne.”
Kulingana na Erdogan, ni muhimu kwa jumuiya ya Kiislamu kuondoa tofauti zao na kuungana kutetea haki za Wapalestina na Walebanoni.
"Ni muhimu sana kwa ulimwengu wa Kiislamu kuweka tofauti zao kando na kuwaunga mkono watu wa Palestina na Lebanon," alisema Erdogan.
Alikosoa utawala wa Kisayuni na wafuasi wao kwa kile alichokiita manyanyaso ya zaidi wa mwaka mmoja, huku akiwapongeza Wapalestina kwa ujasiri wao.
Kama sehemu ya kuguswa na hali mbaya ya kibindamu, Erdogan alibainisha kuwa zaidi ya tani 85,000 za misaada zimewasilishwa Gaza kutoka Uturuki kwa ushirikiano kutoka kwa mamlaka za Misri.
Aliongeza kuwa kutambulika kimataifa kwa dola ya Kipalestina, kutatuma ujumbe wa nguvu kutokana na unyanyasaji wa Israeli unaoendelea dhidi ya Gaza na Lebanon.
Kauli ya kiongozi huyo wa Uturuki inakuja wakati uvamizi wa majeshi ya Israeli huko Gaza ukiendelea, licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka kusitishwa kwa mapigano.
Kulingana na maofisa wa afya wa eneo hilo, zaidi ya watu 43,300—wengi wao wakiwa wanawake na watoto—wameuawa, na wengine zaidi ya 102,000 wamejeruhiwa. Kwa sasa, Israeli inakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuhusu matendo yake huko Gaza.