Kuteuliwa kwa Tanzania, Kenya na Uganda kuna maanisha nchi hizi tayari moja kwa moja zimefuzu kwa ajili ya michuano hii kwa kigezo cha kuwa wenyeji.  / Picha :  X -Janet Museveni 

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameongoza wananchi wake katika kushangilia kukabidhiwa kwa Afrika Mashariki shughuli ya kuandaa kombe la taifa bingwa Afrika Afcon 2027.

Tanzania, Kenya na Uganda ziliwasilisha ombi la pamoja huku wakishindania fursa hiyo na wapinzani Misri, Senegal na Botswana.

"Tunamshukuru Mwenyezi Mungu tumefanikiwa kuwa wenyeji wa michuano mikubwa ya soka Afrika (AFCON2027), tukishirikiana na Kenya na Uganda," alisema Rais Samia katika mtandao wa X.

Kwa Upande wake Rais wa Kenya WIlliam Ruto aliwapongeza wizara za michezo za Afrika Mashariki kwa kuonesha ushirikiano katika ombi hilo.

''Watu wengi hawakuamini kuwa tungepewa fursa hii na kuwa tunao uwezo wa kuandaa kombe hilo kutokana na hali ya soka katika nchi zetuna miundo mbinu. lakini najivunia sana leo kwa kuwa Kenya, pamoja na ndugu zetu wa Tanzania na Uganda tumeonesha umahiri wetu na kunyakua haki yatu ya kuandaa kombe hilo,'' amesema Rais Ruto.

Marais hao wamewachagiza wadau wote wa mpira wa soka Afrika Mashariki kuwajibika na kuhakikisha kila kitu kinawekwa sawa.

''Nawaagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhakikisha tunafanya maandalizi mazuri, ikiwemo kukamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu, viwanja viwili vipya vya kisasa vya michezo Arusha na Dodoma," ameandika Rais Samia kupitia akaunti yake ya X, zamani Twitter.

Mashirikisho ya soka katika nchi hizo pia zimepongeza hatua hiyo kama ushindi wa soka ya Afrika Mashariki.

Rais wa Kenya alisisitiza kuwa sasa ni jukumu lao kama waandaaji kuhakikisha wanatoa mtanange wa kiwango cha kimataifa 'kisichosahaulika.'

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa nchi hizi za Afrika ya Mashariki kuandaa michuano hii toka ianzishwe 1957.

Rais wa CAF Patrice Motsepe amezitangaza nchi hizi kuwa wenyeji baada ya Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo kukutana leo Septemba 27, 2023 mjini Cairo, Misri.

Kuteuliwa kwa Tanzania, Kenya na Uganda kuna maanisha nchi hizi tayari moja kwa moja zimefuzu kwa ajili ya michuano hii kwa kigezo cha kuwa wenyeji.

TRT Afrika