Mechi ya ufunguzi wa michuano ya African Super League kati ya wenyeji Simba Sports Club ya Tanzania na mabingwa mara zote wa ligi ya Mabingwa barani Afrika Al-Ahly uliandaliwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Tanzania. Picha: Simba

Na Suleiman Jongo

Siku kadhaa baada ya klabu ya Simba ya Tanzania kutawala mazungumzo kila kona ya jiji la Dar es Salaam juu ya ufunguzi wa hali ya juu na kiwango bora cha mechi hiyo, macho yote leo yako Misri, ambapo Simba imetua ugenini kwa mechi ya marudio.

Wageni mbalimbali mashuhuri walikuwepo Tanzania wakiwemo Rais wa shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino na Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Patrice Motsepe katika uwanja wa Mkapa, uliofanyiwa marekebisho makubwa na kupambwa kila kona kwa nembo maalum za ‘African Super League’ kutoka shirikisho la soka barani Afrika (CAF).

Aidha, aliyekuwa meneja wa klabu ya Arsenal ya Uingereza, Arsene Wenger, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya soka Duniani alikuwa ni sehemu ya ugeni mkubwa wa mashindano hayo, yaliyofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika.

Rais wa FIFA, Infantino, kocha wa zamani wa Arsenal, Arsène Wenger na rais wa soka Tanzania TFF Wallace Karia wakijumuika na Simba baada ya mechi ya African Football League mjini Dar Es Salaam. Picha: Simba SC Tanzania

Mshindi wa mechi ya leo atatinga nusu fainali kukabiliana na mshindi wa mechi kati ya Mamelodi Sundowns na Petro Atletico. Sundowns ilijipatia ushindi wa 2-0 katika mechi ya awali kati ya pande hizo.

Kuelekea mechi yao ya marudio, kocha mkuu wa Simba Roberto "Robertinho" Oliveira, ameahidi kuimarisha kikosi chake na kufanya mabadiliko tofauti na wale waliopambana na Al Ahly nyumbani Dar es Salaam.

“Ninafahamu tutakuwa na mechi ngumu dhidi ya timu kubwa Afrika ila kuna namna ambavyo tutaingia na mpango tofauti na ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza nyumbani. Nitakuwa na mabadiliko ya wachezaji kwenye baadhi ya maeneo ili kufanikiwa kucheza vizuri na kupata ushindi." Kocha mkuu Roberto "Robertinho" Oliveira, alisema.

"Soka ni mchezo wa wazi na wala si rekodi zilizopita. Kwa upande wetu tumefanya maandalizi ya kutosha kulingana na mahitaji ya mchezo wetu ulivyo na lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunapata matokeo mazuri. Hali na morali ya wachezaji zipo juu na hili linawezekana kulitimiza," Staa wa Simba willy Essomba Onana amesema.

Mashabiki wa Simba, mabingwa wa zamani nchini Tanzania wamekuwa na hamasa kubwa ya kutaka kuendeleza tena ubabe dhidi ya Mafarao wakiwa ugenini huku wakisema historia inaonyesha Al-Ahly hawajawahi kuifunga Simba katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ingawa licha ya kauli mbiu yao ‘kwa Mkapa hatoki mtu salama’ ndani ya dakika 90, wikendi iliyopita, timu hizo zilipokutana Simba haikufanikiwa kurudia historia ya kumfunga Al-Ahly walipochuana Ijumaa Oktoba 20.

Luis Miquissone staa wa Msumbiji, alifunga goli lililoiwezesha Simba kuifunga Al-Ahly 1-0 katika mechi ya ligi ya Mabingwa barani Afrika iliyochezwa katika uwanja wa Mkapa 2021. Picha: Simba SC

Je Miquissone atarudia tena alichokifanya 2021?

Luis Miquissone staa wa Msumbiji, aliyefunga goli lililomfanya asajiliwe na Al-Ahly kabla ya sasa kurejea tena Msimbazi atakuwa anatagemewa na timu yake kwani bao hilo lake ndilo liliiwezesha Simba kuifunga Al-Ahly 1-0 katika mechi ya ligi ya Mabingwa barani Afrika iliyochezwa katika uwanja wa Mkapa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000.

Historia ya simba dhidi ya al-ahly uwanja wa nyumbani

Klabu ya Simba iliyoanzishwa mnamo 1936, imefanikiwa kuifunga Al-Ahly mara tatu katika historia yao kwenye michuano ya ligi ya Mabingwa barani Afrika, hivi karibuni.

Mwaka 1985 Simba ilishinda Al Ahly 2-1, na kuifunga tena Al Ahly 1-0 mwaka 2019, na waliwafunga tena 1-0 mwaka 2021.

Lakini pia, Al-Ahly wamekuwa na rekodi ya kibabe wanapocheza na Simba wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani, ukiwemo ushindi wa 5-0 mwezi Februari, 2019.

Awali, baadhi ya mashabiki wa Simba jijini Dar es Salaam, waliitetea timu yao wakiwa na matumaini makubwa kuelekea mechi hiyo huku wakiieleza TRT Afrika Swahili matarajio yao.

“Mechi kati ya Al-Ahly na Simba ni mechi kubwa barani Afrika. Ni burudani kubwa ya soka nchini Tanzania. Kila mtu anaitamani mechi hii, wakiwemo mashabiki kutoka mikoa mbalimbali nchini na hata nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda na kwingineko duniani. Sako Simba, shabiki kindakindaki wa klabu ya Simba,” alieleza akiwa amejawa na shauku.

“Nimesafiri na Simba hadi Uganda na Zambia kwenye michuano ya kimataifa,” amesema shabiki Hamis Migoma kutoka tawi la Simba la Mpira Mpesa anayeishi Mburahati Madoto.

“Tuna hamasa kubwa ambayo haijapata kutokea katika historia ya soka,” alisema.

Kikosi cha AL Ahly ya Misri kabla ya mechi yake na Simba, nchini Tanzania. Picha AL Ahly.

Al Ahly tayari kwa Simba

Mshindi wa ligi atapokea tuzo ya dola milioni 4.

Said Mpaluka ni shabiki mwingine kutoka Mtoni Mtongani ambaye anasema Al-Ahly ni timu kubwa barani Afrika, lakini kipigo ni kikombe cha bati cha moto wasichokiepuka.

Ahly wamepata nafuu baada ya beki wa kushoto wa Tunisia Ali Maaloul ambaye alikosa mechi ya kwanza pamoja na beki Mohamed Abdel-Moneim kurejea kwani wote wamepona majeraha ya mguu.

Kocha wa Ahly, Mswisi Marcel Koller amejutia nafasi walizopoteza katika mechi ya kwanza lakini bado anaamini kuwa matokeo yao yatakuwa mazuri. "Tulifanya vizuri katika kipindi cha kwanza na kukosa nafasi kadhaa za kufunga bao. Katika kipindi cha pili, tulirudi nyuma na kuruhusu Simba kurudi kwenye mchezo", Koller alisema kwenye kikao na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa leo.

Kombe la AFL, lililoanzishwa na Shirikisho la soka Afrika (CAF) kwa ushirikiano na FIFA, linajumuisha timu nane bora kutoka bara lote, ikiwa pamoja na Tp Mazembe ya DR Congo, Esperance kutoka Tunisia, Enyimba kutoka Nigeria, na Wydad ya Morocco.

TRT Afrika