Klabu ya Simba Sports Club, Tanzania, itawakilisha Ukanda wa Kusini-Mashariki baada ya kujumuishwa pamoja na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, na Atlético Petróleos de Luanda kutoka Angola.
Simba ndio timu pekee ya Afrika Mashariki kama sehemu ya timu 8 maarufu na zilizofanikiwa zaidi barani Afrika kutoka Mikoa 3 ya Kanda ya Afrika ambayo ni: Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati-Magharibi na Kanda ya Kusini-Mashariki.
Klabu ya Al Ahly ya Misri, Espérance Sportive de Tunis ya Tunisia na Wydad Athletic Club kutoka Morocco ni vilabu vya kandanda kutoka Kanda ya Kaskazini. Miamba wa Soka, Enyimba ya Nigeria na Tout Puissant Mazembe ya DRC ndio Vilabu kutoka Ukanda wa Kati-Magharibi.
Ligi hiyo ya Soka ya Afrika (AFL) imeundwa ili kuonyesha wachezaji bora wa soka wa klabu za Afrika na kuwapa mashabiki wa kandanda barani Afrika na ulimwengu mzima, fursa ya burudani, kwa kuona na kufurahia mchezo bora kabisa katika Bara la Afrika.
Sherehe ya uzinduzi wa shindano hilo la kihistoria la AFL na mechi ya kwanza itafanyika tarehe 20 Oktoba 2023 jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Mashindano hayo yataanza kwa hatua ya robo fainali yakifuatiwa na nusu fainali itakayofanyika kati ya tarehe Oktoba 29 na Novemba 1. Fainali zitakazoamua mshindi wa shindano la Uzinduzi wa AFL zitafanyika tarehe 5 na 11 Novemba 2023.
Ratiba ya mashindano ya kwanza ya AFL, ambayo ni ushirikiano kati ya CAF na FIFA imeundwa kwa misingi ya mechi za nyumbani na ugenini na itaanza kwa hatua ya robo fainali ya mtoano.