Michuano hiyo itakayoendelea kwa muda wa wiki moja, inashirikisha timu tisa Picha: CECAFA

Michuano ya kumsaka mwakilishi wa shirikisho la soka ukanda wa Afrika Mashariki CECAFA kwenye fainali za kombe la CAF kwa wanawake imeanza rasmi nchini Uganda huku jumla ya timu tisa wakiwemo mabingwa wa ligi mbalimbali ya kina dada wakiingia uwanjani Kampala.

Kulingana na ratiba ya mechi hizo, hii leo wawakilishi wa Kenya, Vihiga Queens watakwatuana na New Generations FC kutoka Zanzibar huku JKT Queens wa Tanzania wakishuka dimbani dhidi ya AS Kigali Women ya Rwanda kwenye mechi zitakazopigwa uwanja wa MTN-Omondi, Lugogo.

Michuano hiyo itakayoendelea kwa muda wa wiki moja, inashirikisha timu tisa zikiwemo Kampala Queens ya Uganda, FAD ya Djibouti, CBE ya Ethiopia, Buja Queens ya Burundi, Yei Joints ya Sudan Kusini zitakazomenyana kuwania nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya CAF inayotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu nchini Côte d'Ivoire.

Siku ya Jumamosi Fazila Ikwaput wa Kampala Queens aliondoka na mpira wa mechi baada ya kufunga hetriki dhidi ya Yei Joint Stars ya Sudan Kusini na kuondoka na ushindi wa 3-0.

Fazila Ikwaput wa Kampala Queens anaongoza jedwali la ufungaji magoli kufuatia mabao yake 3 dhidi ya Yei Joint Stars FC. Picha: FUFA

Wakati huo huo, Benki ya Biashara ya Ethiopia CBE FC waliotua fainali ya makala yaliyopita, walitoka na ushindi wa 2-1 dhidi ya BUJA Queens wa Burundi huku wakichukua pointi tatu muhimu kwenye Kundi A. Mechi zote zilichezwa katika Kituo cha Ufundi cha shirikisho la Soka Uganda, FUFA, Njeru.

Mechi za Kundi A zitaendelea tena Jumanne wiki ijayo huku wenyeji Kampala Queens wakicheza na BUJA Queens nao FAD FC kutoka Djibouti wakimenyana na CBE FC.

TRT Afrika