Simba SC imeeleza nia yake ya kuendeleza ushirikiano zaidi wa sekta ya spoti na timu kubwa kama Galatasaray huku ikasema ya kwamba uhusiano wa nembo zao katika kumtumia mnyama Simba ni kielelzo tosha.
Viongozi wa Klabu ya Simba SC ya Tanzania wakiongozwa na mwenyekiti wa bodi Salim Abdallah (Try Again) walifika ubalozini hapo na kukaa chini kuzungumza mambo mbali mbali.
Kambi iliyowekwa na Simba SC katika mji mkuu wa Uturuki Ankara kwa takriban majuma matatu imeonekana kuzaa matunda, kwani wekundu wa msimbazi hao hawajapoteza mechi hata moja kati ya michezo 6 waliocheza na kunyakua kombe la ngao ya jamii kwa kuwalaza mahasimu wao wa jadi wa enzi na enzi Yanga Sports Club.
Aidha, Abdallah aliongeza kuwa kambi yao ilikuwa yenye mafanikio makubwa sana na Simba SC ipo tarayi kushirikiana na timu za Uturuki.
‘’Mimi nahisi ni mwenye bahati, mwaka 2017 au 2018 nilikuwa hapa (ubalozini) balozi aliyepita alitualika. Anaipenda Simba, labda waturuki wanaipenda sana Simba’’ Abdallah aliiambia TRT Afrika.
Abdallah alikumbusha ya kwamba mnamo mwaka 2017 Simba SC walialikwa na ubalozi wa Uturuki nchini, na waliwahi kuweka kambi Uturuki hapo kabla, lakini kambi ya mwaka huu imekuwa na mafanikio zaidi.
Balozi Mehmet Güllüoğlu amesema yuko tayari kukuza ushirikiano hasa katika kuimarisha mahusiano baina ya timu za Tanzania na Uturuki na kuongeza kuwa mabadilishano ya wanamichezo, mbali na mpira wa miguu yanaweza kuhusisha na kukuza mahusiano baina ya nchi na raia wa pande hizo mbili.
Akigusia mfano wa mchezaji Mbwana Ally Samatta aliyekipiga kwenye timu ya Fenerbahçe alikuwa tayari ni sababu ya Tanzania kujulikana zaidi baina ya mashabiki wa soka Uturuki. ‘
’Tutakaa chini na kujadiliana juu ya namna ya kujenga ushirikiano na kukuza mahusiano ya kibiashara’’ Güllüoğlu alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Simba SC, Imani Kajula, ameisifia kuwa kambi yao ya Uturuki ndio kambi bora zaidi kuwahi kufanyika kwa timu ya Simba SC kwa mujibu wa mapokezi, na huduma mbalimbali akitaja kila kitu kilikuwa kizuri sana kufikia hadi waliporudi Tanzania.
Murtaza Mangungu mwenyekiti wa timu, amesema alikwenda Ankara kwenye kambi ya Simba na kukaa kwa muda wa siku 9 huku akiweka wazi kuvutiwa kwake na mandhari ya eneo hilo kuanzia huduma za hoteli, viwanja vya mazoezi na hata hali ya hewa ilikuwa rafiki sana kwa maandalizi ya timu yao.
Simba SC kushirikiana na magwiji wa Uturuki.
Mkutano huo ulijadili namna ya kukuza ushirikiano wa kimichezo baina ya Uturuki na Tanzania. Abdallah alikumbusha ya kwamba mnamo mwaka 2017 Simba SC walialikwa na ubalozi wa Uturuki nchini, na waliwahi kuweka kambi Uturuki hapo kabla, lakini kambi ya mwaka huu imekuwa na mafanikio zaidi.
Simba imeahidi kuendelea kuichagua Uturuki kama kambi yake ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu. Baada ya mkutano huo Simba SC walitoa jezi za msimu mpya kama zawadi kwa Balozi na watumishi wake.