Klabu ya soka ya Tanzania Simba, maarufu 'Wekundu wa Msimbazi', wameanza kambi ya mazoezi nchini Uturuki kujinoa kwa msimu ujao.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amefafanua kuwa timu hiyo itakuwa Uturuki kwa muda wa majuma matatu kufanya matayarisho kabambe ikiwemo kupiga mechi za kirafiki na timu mbalimbali za Uturuki.
“Tukiwa Uturuki tutakaa kambi ya siku 21 na tutarejea Tanzania tarehe moja mwezi wa nane. Tutacheza mechi tatu za kirafiki na tutaeleza ratiba ya mechi hizo hapo baadaye.” Alisema Ahmed Ally.
Licha ya kuchujwa 4-3 na Wydad Atheltic Club ya Morocco, kupitia penalti kwenye hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika CAF, Simba, imeonyesha nia yake ya kujiandaa vikamilifu msimu ujao kwa kuwanasa mastaa wapya mapema.
Miamba hao wanaoongozwa na Kocha Mkuu Roberto Oliviera ‘Robertinho’, wameimarisha maandalizi yao kwa kuwasajili Willy Essomba Onana ambaye alitunukiwa mchezaji bora msimu huu kwenye ligi kuu ya soka Rwanda na nyota wa Cameroon Che Malone Fondoh na Aubin Kramo.
Nguvu hao mpya watapiga jeki huduma za Saidi Ntibazonkiza aliyezoa tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu 2022/23, kwa magoli 17 pamoja na kuzawadiwa tuzo ya kiungo bora wa Ligi Kuu 2022/23.
Timu hiyo pia imetengana na baadhi ya wachezaji wake wakiwemo mlinzi wa kushoto Gadiel Michael, Erasto Nyoni, mlinda lango, Beno Kakolanya, kiungo mshambuliaji Nelson Esor-Bulunwo Okwa, mlinzi wa kati Mohamed Ouattara, Victor Akpan, kiungo mkabaji Ismael Sawadogo, Jonas Mkude aliyeitumikia kwa miaka 13 na wengineo.
Mbali na kuikarabati kikosi chake cha wachezaji, timu hiyo pia imefanya mabadiliko kwenye benchi lake la kiufundi.
Kocha Kelvin Mandla ambaye alikuwa kocha wa viungo amempisha Corneille Hategekimana huku mtaalamu wa viungo Fareed Cassim akiihama timu hiyo.
Wengine walioondoka ni kocha wa magolikipa, Chlouha Zakaria huku nafasi yake ikichukuliwa na Kocha mpya Daniel Cadena Ledesma.
Mikael Igendia ambaye alikuwa ni mkuu wa sayansi ya michezo, katika timu ya Harambee Stars ya Kenya hapo awali, sasa ndiye meneja mpya wa timu na mkuu wa sayansi ya michezo.