Mechi za kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON) 2024 zinarejea leo huku kina dada wa Afrika mashariki wakitinga uwanjani kwa ajili ya mechi za mkondo wa pili. Picha: Harambee Starlets.

Harambee Starlets ya Kenya na Twiga Stars ya Tanzania zinatarajia kutumia fursa za kuwa nyumbani wanapochuana dhidi ya Cameroon na Cote D'ivore mtawalia.

Kenya inalenga kupindua matpkeo ya kupoteza mechi ya mkondo wa kwanza ugenini 1-0 dhidi ya Cameroon, kwenye mchuano uliratibiwa kupepetwa katika uwanja wa Nyayo Jijini Nairobi.

Beldine Odemba, kocha wa Kenya amewataka mashabiki kuishangilia timu kwa mechi nzima ili kupiga jeki matumaini yao ya kuwa nyumbani.

"Ningependa kuwahimiza waje kwa wingi. Starlets wamekuwa wakipata ushabiki mkubwa kutoka kwa mashabiki, na tunajua wanatuamini, na ikiwa watajitokeza kwa wingi, itakuwa nyongeza kubwa, " ameongeza kocha.

Aidha, Twiga Stars itakuwa kazini katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi dhidi ya Côte d'Ivoire iliyoifunga 2-0 huku ikidhamiria kujinufaisha na faida ya kuwa nyumbani baada ya magoli ya F. Akebie Abrogoua na I. Ida Guehai kuzamisha matumaini yao ugenini.

Kocha wa Tanzania Bakari Nyundo Shime amesema, ingawa wanakabiliwa na timu yenye nguvu ya Cote D'ivoire, wachezaji wake watahitaji kuwa makini zaidi ili kupata matokeo mazuri ya kuwawezesha kutinga raundi inayofuata.

Mechi hizo za kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON) 2024 zinarejea leo huku kina dada wa Afrika mashariki wakitinga uwanjani kwa ajili ya mechi za mkondo wa pili.

Tayari Sudan Kusini imeliaga shindano hilo baada ya kulazwa na Misri katika mechi zake zote mbili 4-0 na kukusanya jumla ya mabao 8-0.

Uganda inatarajia kupata matokeo mazuri katika mji wa Oran baada ya kufungwa 2-1 awali ikiwa nyumbani dhidi ya Algeria katika mechi ya mkondo wa kwanza.

TRT Afrika