Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) Patrice Motsepe./Picha: Wengine

Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limetangaza kuahirishwa kwa michuano ya CHAN 2024, hadi mwezi Agosti 2025.

Makala ya nane ya mashindano hayo ambayo ni maalumu kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani barani Afrika, ilipangwa kuanza Februari 1 hadi Februari 28, ikiandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda.

Hata hivyo, kulingana na wataalam wa CAF, nchi hizo tatu bado zinahitaji muda zaidi kushughulikia miondombinu mbalimbali, ikiwemo viwanja ili ziwe katika nafasi nzuri ya kuandaa mashindano hayo.

Katika taarifa yake iliyotolewa siku ya Januari 14, CAF ilibainisha maandalizi mazuri yaliyofanywa na Tanzania, Kenya na Uganda kuelekea katika mashindano hayo.

“Licha ya mambo mazuri tuliyoyaona, tunadhani ni vyema kwa nchi hizo kupewa muda zaidi wa kujiandaa ili kuweza kuandaa michuano ya CHAN 2024,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Dkt. Motsepe akifanya ukaguzi wa uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam nchini Tanzania./Picha: @Tanfootball

Kwa upande wake, Rais wa CAF Dkt. Patrice Motsepe alitoa pongezi kwa Marais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, William Ruto wa Kenya na Yoweri Museveni wa Uganda kwa uongozi wao dhabiti katika maandalizi ya michuano hiyo, ikiwemo ukarabati wa viwanja, hoteli, hospitali na miundombinu mingine.

“Nimefurahishwa na kasi ya maandalizi. Nina imani kuwa mambo yote hayo yatakuwa tayari ifikapo mwezi Agosti 2025,” alisema Motsepe.

Motsepe akiwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Kenya./Picha: Wengine

Mwezi Disemba mwaka jana, timu ya wakaguzi wa CAF ilikita kambi katika nchi hizo tatu, ikipima maandalizi ya CHAN 2024.

Licha ya kufurahishwa na maandalizi hayo, bado wakaguzi hao waliipa Kenya mpaka Disemba 31, 2024 wawe wamemaliza ukarabati kwenye viwanja vya Moi International Sports Centre,Kasarani na ule wa Nyayo.

TRT Afrika