Mamlaka ya wanyamapori nchini Uganda (UWA) inasema vifaru wawili wa kiume walizaliwa ndani ya siku mbili katika hifadhi ya 'Ziwa Rhino Sanctuary', iliyo zaidi ya kilomita 160 kutoka jiji la Kampala.
Vifaru waliozaa wanaitwa Malaika na Uhuru .
"Hili ndilo jambo ambalo mtu yeyote katika uhifadhi anataka kuona, tumetoka mbali tangu 1983 wakati vifaru walipotoweka nchini Uganda, juhudi zetu za kuwatambulisha na kuwazalisha vifaru zipo wazi kwa kila mtu kuona," mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya UWA Sam Mwandha alisema katika taarifa.
Mwaka 2006 mama wa vifaru wawili ambao wamezaa, aliletwa nchini kama zawadi kutoka kwa ‘Disney's Animal kingdom’ huko Marekani.
Aliletwa pia na kifaru mwingine dume.
Mamlaka ya wanyamapori nchini Uganda (UWA), linasema kuzaliwa kwa vifaru hao wawili kumeongeza idadi ya vifaru katika eneo la hifadhi la Ziwa Rhino Sanctuary kuwa 38.
Eneo hilo lilianzishwa mwaka 2005 kwa lengo la kurudisha idadi ya vifaru weupe nchini Uganda.