Nchi za Ghuba zimewashauri raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Tanzania na Equatorial Guinea kutokana na virusi vya Marburg katika nchi zote mbili.
"Tunawashauri raia wetu kuahirisha safari ya Tanzania na Equatorial Guinea, ambako virusi vya Marburg vimegunduliwa," ilisoma taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE siku ya Jumamosi.
Mamlaka ya Imarati pia imewataka raia wao walioko Tanzania na Equatorial Guinea kuwa waangalifu na kufuata maagizo ya usalama yanayotolewa na mamlaka hiyo.
Wizara ya Afya ya Kuwait kupitia taarifa yake pia iliwashauri raia wake kuepuka kusafiri kwenda Tanzania na Equatorial Guinea hadi pale virusi vya Marburg vitakapodhibitiwa katika nchi zote mbili. Raia wa Kuwait katika nchi hizi na jirani wameshauri kufuata hatua zinazotolewa na mamlaka ya afya ya eneo hilo.
Wizara ya Afya ya Bahrain iliripoti kwamba maendeleo ya hali kuhusu virusi vya Marburg yanafuatiliwa kwa karibu na kwamba hatari ya uhamisho wa virusi hivyo hadi Bahrain bado ni ndogo.
Hakika, hakuna safari za ndege za moja kwa moja kutoka Tanzania na Equatorial Guinea hadi Bahrain.
Saudi Arabia na Oman wamechukua hatua sawa na wenzao. Mamlaka ya afya ya Saudi Arabia imewashauri raia wao kutosafiri katika nchi hizi hadi mlipuko wa virusi vya Marburg utakapodhibitiwa.
Wizara ya Afya ya Oman ilisisitiza katika taarifa kwamba virusi vya Marburg vinaambukiza 60-80%. Taarifa hiyo hiyo iliwataka raia wa Oman kutosafiri kwenda Tanzania na Equatorial Guinea, isipokuwa katika hali ya lazima.
Virusi vya Marburg viligunduliwa kwa mara ya kwanza mnamo 1967 katika maabara huko Marburg, Ujerumani. Huambukizwa na popo wa matunda na kwa binadamu kupitia majimaji ya mwilini au kugusana na watu walioambukizwa.
Dalili kama vile homa kali, maumivu makali ya kichwa, uchovu na kutapika huonekana ghafla kwa watu walioambukizwa, na wagonjwa wengi hupata dalili za kutokwa na damu katika sehemiu za mwili ndani ya siku saba.
Hakuna chanjo au matibabu maalum, na virusi vinaweza kusababisha kiwango cha vifo cha hadi 90%.
Asilimia 90 ya watu 252 walioambukizwa virusi vya Marburg walikufa wakati wa janga la 2005 nchini Angola.