Serikali ya Kenya imefanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri lililowaathiri mawaziri saba kupitia tangazo lililotolewa na Ikulu ya Kenya.
Musalia Mudavadi ambaye ni Katibu Mkuu wa Mawaziri, ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya nje huku waziri wa awali aliyekuwa akishikilia kitengo hicho, Alfred Mutua akihamishwa kuwa Waziri mpya wa Utalii na Wanyamapori.
Kwenye badiliko jengine, aliyekuwa waziri wa Utalii, Peninah Malonza ndiye Waziri mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Maeneo Kame na Maendeleo ya Kikanda.
Wakati huo huo, Waziri wa zamani wa wizara hiyo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Maeneo Kame na Maendeleo ya Kikanda Rebecca Miano ndiye ametangazwa kuwa Waziri mpya wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda.
Aidha, uteuzi huo, umemuathiri Waziri Moses Kuria ambaye amehamishwa kutoka Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda na kuwa Waziri mpya wa Utumishi wa Umma, Utendaji na Usimamizi wa Utoaji.
Katika Mabadiliko hayo, yaliyotolewa na Msemaji wa Ikulu ya Kenya, Hussein Mohamed, waziri wa zamani wa Maji, Usafi wa Mazingira na Umwagiliaji, Alice Wahome ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Vile vile, Zachariah Mwangi Njeru ameteuliwa kuwa Waziri wa Maji, Usafi wa Mazingira na Umwagiliaji, huku wakipishana na Alice Wahome.
Waziri wa zamani wa Utumishi wa Umma, Aisha Jumwa Katana, ameteuliwa kuwa Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi.
Orodha kamili ya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri
- Musalia Mudavadi - Katibu Mkuu wa Mawaziri, na Waziri wa Mambo ya Nje
- Alice Wahome - Waziri wa Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
- Rebecca Miano - Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda
- Moses Muria - Waziri wa Utumishi wa Umma, Utendaji, na Usimamizi wa Utoaji
- Alfred Mutua - Waziri wa Utalii na Wanyamapori
- Aisha Jumwa Katana - Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi
- Zachariah Mwangi Njeru - Waziri wa Maji, Usafi wa Mazingira na Umwagiliaji
- Peninah Malonza - Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Maeneo Kame na Maendeleo ya Kikanda
Mbali na mabadiliko ya uhamisho wa mawaziri, rais William Ruto pia ameonekana kutetemesha wizara mbalimbali na kuhamisha baadhi ya vitengo kutoka wizara moja hadi nyingine.
Kwa mfano, Idara ya Sanaa imenyofolewa kutoka Wizara ya Michezo huku Idara nyingine ya Urithi ikiondolewa kutoka Wizara ya Utalii.
Waziri wa zamani wa biashara Moses Kuria ameongozewa idara ya Utendaji na Usimamizi wa Utoaji kwani awali, Wizara hiyo ilikuwa ikiitwa Wizara ya Utumishi wa Umma na Jinsia.