Wabunge Kenya watajadili kwa mara ya pili mswada wa fedha 2023 ambao unalenga kuongeza mapato ya kindani  / Photo: Reuters

Na Coletta Wanjohi

Zoezi la kujadili Mswada wa Fedha wa 2023 uliyotarajiwa kujadiliwa leo bungeni kwa mara ya pili umeahirishwa hadi tarehe 13 Juni kwa sababu bunge limesema haikuwa tayari kwa ajili ya suala hilo.

Serikali ya William Ruto inataka kuongeza ufadhili wa ndani kwa kufanya marekebisho kwa baadhi ya sheria za kodi.

Mswada huo unapendekeza mabadiliko ambayo yanalenga kuongeza ushuru na kuongeza mapato ili kukidhi bajeti kuu ya serikali ya zaidi ya dola bilioni 25 za marekani kwa mwaka wa 2023/2024.

Vipengengele kadhaa katika mswada huo vimezua utata nchini huku watu wengine wakilaumu serikali kwa kuongeza ushuru huku mapato ya watu ni duni na gharama ya maisha iko juu.

Kumekuwa na maandamano kadhaa na wananchi wakitaka serikali kuondoa mswada huo bungeni.

Kwa mfano mswada wa Sheria ya Fedha unapendekeza kuanzishwa kwa mfumo ambapo wafanyakazi watatakiwa kusalimisha asili mia 3 ya mishahara yao na wafanyakazi hao asilimia 3 nyingine ili kufadhili mfumo wa nyumba ambao utaiwezesha nchi kujenga angalau nyumba 250,000 kwa mwaka.

Unapendekea kiwango cha ushuru cha asili mia 35 kwa wale wenye mapato zaidi ya Kshs 500,000, (3600 USD), kwa mwezi.

Inataka waundaji wa maudhui dijitali watozwe asili mia 15 ya kodi kwa mapato yanayopatikana.

Kinara wa Upinzani Raila Odinga amemtaka rais Willaim Ruto kunyenyekea na kuondoa mswada wa fedha na kuomba msamaha kutoka kwa Wakenya.

Mswada unataka kuongezeka kwa kiwango cha kodi kwa bidhaa za kwenye bidhaa za petroli kutoka asilimia 8 hadi asilimia 16.

Kinara wa upinzani nchini Kenya , Raila Odinga amemtaka rais ruto 'kujinyenyekea na kuondoa mswada huo bungeni na baadaye kuwaomba wakenya msamaha'.

"Mswada huu wa fedha ni kama ugonjwa ambao hauwezi kuponywa kwa mitishamba ya kila siku," Odinga, kiongozi wa muungano wa Azimio amesema.

" Mswada wa Fedha unaonekana kujaribu kutatua tatizo tulilo nalo kwa kukusanya mengi zaidi na kujaribu kupata matumizi," anasema John kinuthia meneja wa miradi katika shirika la International Budget Partnership Kenya (IBPK).

" Iwapo hatutatua changamoto ya matumizi na vipaumbele tuliyo nayo, haijalishi ni mapato kiasi gani tunayojaribu kukusanya kwa Mswada huu wa Sheria ya Fedha, hatutatoka kwenye fujo tuliyomo."

Mtaalamu wa Sheria Patrick Lumumba katika mtandao wake wa twitter amesema

"Kwa bahati mbaya, Wakenya wengi wanaopiga kelele zaidi hawajasoma waraka huo. Ninawasihi Wakenya wote wenye nia njema kusoma kabla ya kutoa maoni.”

Mswada huu ililetwa bungeni na serikali mara ya kwanza mnamo tarehe 28 Aprili 2023.

Ikipitishwa na bunge, itarejea tena isomwe upywa na mabadiliko ambayo yatakuwa yamefanywa.

Baadaye rais ataidhinisha sheria na hapo kuanza kutimika kwa sheria hio tarehe mosi mwezi Julai ambayo ndiyo mwanzo wa mwaka wa kifedha nchini Kenya.

TRT Afrika