Bunge la Kenya limepokea mswada wa Fedha wa 2023 kujadiliwa kwa mara ya pili.
Mjadala wa wabunge ulikuwa mkali sana huku wabunge wanaopinga wakidai mapendekezo yake yata ongeza gharama ya maisha kwa Wakenya.
Baada ya ushirikishwaji wa umma serikali imefanya marekebisho kadhaa kwa mapendekezo yao ya awali kwa nia ya kulishawishi baraza hilo kuunga mkono mswada huo.
Pendekezo la kuanzishwa kwa ushuru mpya ya nyumba lilizua utata huku baadhi ya wananchi wakisema kuwa hawataki kuchangia asilimia 3 ya mishahara yao kwenye mfuko wa wa nyumba wa serikali, waajiri wao wangetarajiwa kuchangia kiasi hicho hicho.
Hii sasa imepunguzwa hadi 1.5%.
Waundaji wa maudhui ya kidijitali pia walikuwa wamekanusha ushuru mpya wa 15% kwenye mapato yao, serikali imependekeza ipunguzwe hadi 5%.
Ushuru unaohusiana na petroli unasalia katika kiwango cha awali kilichopendekezwa cha asilimia16%.
Mbunge wa Suna Magharibi Masara Peter alisema ingawa bajeti lazima ifadhiliwe na mapato ya ndani ya nchi, muda wa kufanya mabadiliko ya mfumo wa kodi nchini sio sasa.
“Petroli ni muhimu kwa uzalishaji kwa jumla kwa hivyo, ukiongeza bei ya mafuta mambo mengine yote yataongezeka maana wanaofanya uzalishaji wataongeza bei."
Serikali pia imerekebisha pendekezo lake la ushuru kwa watu wanaopata kati ya dola 3600 na 5,700.
Mapendekezo ya awali kwamba walipwe ushuru 35% ya mapato yao yamepunguzwa hadi 32.5%.
Wale wanaopata 800,000 sasa watalazimika kulipa 35% ya mapato yao kama ushuru.
Otiende Omollo mbunge wa Rarieda alisema mswada huo ni njia ya kutoza ushuru kupita kiasi.
"Sielewi jinsi serikali ambayo tayari inasema kuna tatizo, inasisitiza kuongeza bajeti ya serikali kutoka zaidi ya dola bilioni ishirini na tatu, hadi zaidi ya dola bilioni ishirini na sita kama inakiri hakuna fedha."
"Muswada huu sio tu kwamba unaangalia mambo ya kujenga nyumba, utafanya mabadiliko ya rasilimali zetu za ndani, utaongeza uzalishaji wa ndani na kwa hivyo tunashughulikia masuala makubwa," Murathania Rindikira Mbunge eneo la Buuno alisema, huku akiunga mkono muswada huo.
Ikipitishwa bungeni, muswada ulioidhinishwa na uliorekebishwa utaidhinishwa na rais na kutekelezwa kuanzia tarehe 1 Julai 2023.