Kwa mujibu wa barua rasmi iliyotolewa na Mkuu wa Utumishi wa Umma nchini Kenya Felix K. Koskei, nchi hiyo imepiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma wa ngazi za juu wakiwemo mawaziri na katibu wa wizara mbalimbali na kupunguza ujumbe unaoandamana na viongozi katika safari za nje.
Hatua hiyo inadaiwa kulenga kuhakikisha utekelezaji wa matumizi bora ya fedha za umma.
Uamuzi huo mpya pia umewaathiri rais, mkewe, naibu wa rais na katibu mkuu wa Baraza la Mawaziri baada ya ujumbe unaoandamana nao kupunguzwa kwa asilimia hamsini na kuwaacha wale wanaoshikilia jukumu muhimu katika ziara pekee.
Aidha, ujumbe unaohusisha waziri na katibu mkuu, umepunguzwa hadi watu watatu pekee huku idadi ya siku za kusafiri pia zikipunguzwa hadi siku saba ikiwa ni pamoja na tarehe za kusafiri.
Mikutano na hafla zilizofadhiliwa, ambazo mara nyingi husababisha nyongeza ya gharama kutoka kwa serikali, ikiwemo marupurupu na tiketi, pia zimesimamishwa, huku afisa aliyealikwa akihitajika kujilipia kiasi cha fedha kinachotarajiwa.
Mashirika ya umma ambayo yamepangwa kusafiri na kuhudhuria hafla, ziara za utafiti, mafunzo, makongamano, maonyesho na mikutano ya uanachama, zinahitajika kuomba ushiriki kwa njia ya mtandao, au kushirikisha Wizara ya Mambo ya Nje ili kupata ushiriki wa maafisa wa kidiplomasia katika nchi husika.
Mwenyekiti au mtendaji mkuu wa mashirika ya serikali atalazimika kusafiri pekee yake bila walinzi au wasaidizi binafsi.
Aidha, ubalozi wa Kenya katika nchi za nje umepewa jukumu la kuhudhuria kikamilifu, na kuwakilisha serikali ya Kenya kabla ya ushiriki wa wizara.
Wizara ya Mambo ya Nje na idara ya uhamiaji zimeamrishwa kuhakikisha utekelezaji wa tangazo hilo kikamilifu.