Watumiaji wa mitandao ya kijamii wakiwemo wasanii mbalimbali nchini Kenya wataanza kupokea mapato kupitia mitandao ya kijamii inayomilikiwa na Meta.
Mitandao hiyo ikiwa ni pamoja na Facebook na Instagram, imetangaza rasmi kuwa kuanzia tarehe 1 Juni 2024, Wakenya wakiwemo wasanii, wachekeshaji na wengineo wataanza kupata malipo chini ya mfumo wa 'monetization'.
Hayo yaliafikiwa kwenye mkutano uliofanyika Ikulu ya Kenya, Nairobi kati ya Rais wa Kenya William Ruto na wasimamizi wa Facebook wakiongozwa na rais wa Facebook wa masuala ya kimataifa Nick Clegg.
"Ni jambo la kufurahisha sana kuona ufanisi wa mpango huu wa kusaka mapato kupitia Facebook na naishuruku kwa kuwezesha hili," amesema rais wa Kenya William Ruto.
"Pia, kuanzia mwezi Juni, malipo kwa wasanii na watumbuizaji wengine yatafanywa kupitia njia ya malipo ya simu, M-Pesa, " Ruto ameongeza.
Kwa upande wao, wawakilishi wa Facebook wamesema kuwa miongoni mwa watakaoanza kupokea malipo kutokana na kurasa zao ni lazima watimize masharti mbalimbali ikiwemo kuwa na wafuasi 5,000 au zaidi kwenye kurasa hizo.