Shughuli za kupakia na kupakua mizigo zikiendelea ndani ya Bandari ya Mombasa./Picha:  @Kenya_Ports

Bandari Kuu ya Mombasa nchini Kenya imeongeza uwezo wa kuhudumia mizigo kutoka tani milioni 35.98 mwaka 2023 hadi tani milioni 41.1 kwa mwka 2024.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) William Ruto, hatua hiyo inafuatia ongezeko la ujazo wa mizigo bandarani humo.

Ruto aliongeza kuwa baadhi ya kampuni kubwa za meli zilichagua bandari ya Mombasa kama kitovu cha kusafirishia na kupokelea mizigo.

“Bandari ya Mombasa inasalia kuwa eneo muhimu la kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na hatua hii kubwa tuliyopiga ni dhihirisho la kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika,” Ruto alisema wakati akizungumza na waandishi wa habari katika jiji la Mombasa.

Kwa mujibu wa Ruto, kitengo cha makontena cha bandari hiyo kilivuka malengo ya kuhudumia makontena milioni 2 yenye urefu wa futi 20 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 10, huku makontena milioni 2.005 yakiwa yameshughulikiwa katika kipindi cha mwaka 2024.

Ruto aliongeza kuwa nchi ya Uganda inasalia kuwa taifa la kwanza lenye kutumia bandari hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki, likiwa limetumia bandari hiyo kupitisha tani milioni 8.81 za mizigo kwa mwaka 2024 kutoka tani milioni 7.11, mwaka 2023.

Nchi nyingine zinazotumia bandari hiyo ni pamoja na Sudan Kusini, DRC, Rwanda na Tanzania.

Ruto alisema kuwa uwekezaji unaoendelea katika bandari hiyo unalenga kuongea ufanisi zaidi wa utoaji huduma katika eneo hilo.

TRT Afrika