Asali ya  Nzarubara ya Grecom inauzwa hadi nje ya  mji wa Goma na sasa inasafirishwa hadi Ujerumani, Ubelgiji  na Marekani. /Picha: Déborah Nzarubara  

Na Firmain Eric Mbadinga

Piramidi za Misri zina siri nyingi, nyingine za kushangaza, na nyingine za ajabu.

2015, wanaakiolojia waligundua vinu vya udongo vya miaka 3,000 vilivyokuwa vimefunikwa na vumbi ndani ya piramidi hizo.

Kilichowashangaza wengi ni yaliyokuwa ndani yake — asali halisi ambayo ilikuwa na ladha yake nzuri na ubora wake licha ya kuwa kwenye sehemu hiyo kwa karne nyingi sana.

Pamoja na kuwa ugunduzi huo ulishangaza watu wa kawaida, kwa wafugaji wa nyuki hawakuona cha ajabu.

Walijuwa kuwa asali ina sifa nyingi, ikiwemo kukaa kwa muda mrefu bila kupoteza ubora wake.

Na ni sifa hizi zilizomvutia Déborah Nzarubara, Mwanamke raia wa DRC kutoka eneo lililokumbwa na vita la mji wa mashariki mwa nchi wa Goma, na kumpa motisha ya kuanza biashara ya ufugaji wa nyuki.

Sweet enterprise Green Community Mind (Grecom), ni kampuni ambayo Déborah alianzisha 2018, na imekuwa ikipanua wigo wake kwa kuimarisha soko, kuongeza wafanyakazi, pamoja na kubuni njia kadhaa za kupata faida.

Nzarubara alianzisha Shirika lisilo la Kiserikali kuwapa mafunzo wafugaji nyuki kuhusu mbinu mpya za kuhifadhi mazingira na kuongeza mavuno ya asali. /Picha: Déborah Nzarubara 

Kupitia mtazamo na juhudi zake za kila siku, Déborah amejitolea kubadilisha fikra hasi katika jamii yake kuhusu ufugaji nyuki wakati huo huo akionesha mbinu za kisasa za ufugaji ambao wengine wanafanya kama suala la kujipumbaza tu.

“Mimi nimezaliwa na kukuwa karibu na mbuga ya Virunga, nimeona wafugaji nyuki wakifanya shughuli zao tangu tukiwa wadogo. Wazazi wangu wenyewe walikuwa wafugaji wa nyuki, na mume wangu pia ni mfugaji. Ukaribu huu umenifanya nione matatizo wanayopata watu walio kwenye biashara hii nchini kwetu. Nafahamu kuwa wakati mwingine wafugaji nyuki huwa wananyanyapaliwa,” Déborah anaiambia TRT Afrika.

“Wengine wanashtumiwa kuwa wachawi kutokana na uwezo wao wa kufuga nyuki. Wengine wanakejeliwa kwa sababu kazi hii kuonekana ni ya watu ambao hawana elimu. Kwa mimi mwenyewe kujifunza na kujihusisha na ufugaji wa nyuki, lengo langu ni kubadilisha mitazamo ya watu kuhusu suala hili.”

Wengine wanashtumiwa kuwa wachawi kutokana na uwezo wao wa kufuga nyuki. Wengine wanakejeliwa kwa sababu kazi hii kuonekana ni ya watu ambao hawana elimu. Kwa mimi mwenyewe kujifunza na kujihusisha na ufugaji wa nyuki, lengo langu ni kubadilisha mitazamo ya watu kuhusu suala hili.

Déborah, ambaye amepata elimu yake ya juu katika chuo kimoja mjini Goma, alifuzu kama mtaalamu mwandamizi, na baada ya hapo akaanzisha shirika lisilo la kiserikali 2013 kuwasaidia wafugaji nyuki.

Shirika hilo la 'Action Solidaire pour la Protection des Abeilles' linawapa mafunzo wafugaji nyuki kuhusu mbinu mpya za kuhifadhi mazingira na kuongeza mavuno ya asali.

“Haya mafunzo yamesaidia sana, na kuwezesha wafugaji wa nyuki kuachana na mbinu ambazo zilikuwa hatari kwa mazingira na uzalishaji wa asali, pamoja na kuwa hatari kwa nyuki pia,” Déborah anaeleza.

Kupanua wigo wake

Utekelezaji wa mbinu zilizoimarika kulisaidia kuimarisha ubora wa asali na uvunaji kwa wingi pia, jambo lililofanya wafugaji kuanza kutafuta masoko zaidi kwa bidhaa hiyo.

Grecom ina bidhaa  nyingi ikiwemo  nta ya nyuki,  na mafuta. /Picha: Déborah Nzarubaru

2018, Kampuni ya Grecom ilianza kutumia mfumo wa kisasa, na wenye kutunza mazingira katika uzalishaji wake wa asali na mauzo.

Wafugaji nyuki walijenga mizinga kwa kutumia vifaa vilivyopatikana kirahisi, wakatengeneza mabomba ya moshi, na kuwa na mavazi sahihi ya kujikinga.

Mbinu mpya na uwekezaji katika vifaa, usafirishaji, na kuimarisha mazingira ya kazi kumehawakikisha matokeo mazuri.

Ubunifu katika mbinu za kutafuta masoko na namna ya kuweka bidhaa kwenye chupa, kumefanya asali halisi ambayo ina virutubisho vyote, kuvutia zaidi kwa wateja.

Wasiwasi wa awali kuhusu asili ya asali hiyo uliondolewa kupitia kampeni zilizofanywa na Grecom.

Ladha ya asali iliyokuwa imefungwa vizuri ndiyo ilivutia zaidi.

"Mkakati wetu umefanikiwa. Tuliwaeleza kuhusu njia tunazotumia wakati wa kuiweka asali kwenye chupa ili kuwa na ubora wa hali ya juu. Hatua kwa hatua watu wakaanza kuamini bidhaa zetu. Sasa tumepata biashara kutoka kwa maduka madogo madogo na makubwa,” anasema Déborah.

Grecom sasa ina bidhaa tofauti ikiwemo nta ya nyuki na hata mafuta ya asali.

Kutoka kwa asili yake mjini Goma, asali ya Grecom imepanua wigo wake hadi kufikia wateja katika miji ya Kinshasa na Bukavu.

Pia inafikia wateja wanayoipenda katika mataifa ya Ujerumani, Ubelgiji, na Marekani.

Kubadilisha mtazamo

Kufanikiwa kwa Déborah kutokana na juhudi zake kumesaidia wafugaji nyuki kuongeza mapato yao na pia kuwaheshimisha katika jamii.

Nzarubara amesaidia kuanzisha vyama vya ushirika kwa wafugaji nyuki jambo lilimfanya atambuliwe na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Barani Afrika. /Picha: Déborah Nzarubara

Programu ya NyukiTech inatambua wafugaji nyuki, kisha kuwasaidia katika kuratibu, kuleta ushirikiano, na fursa za mafunzo kwa sekta nzima ya ufugaji nyuki.

Kila mara wanapeana taarifa kuhusu hatari ya hali ya anga na mbinu za uzalishaji, na mawasiliano kupitia ujumbe mfupi yanasaidia wafugaji nyuki kote katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kusaidiana kadiri wanavyoweza.

Kwa kawaida Déborah, mama mwenye watoto wanne, huwa hajikwezi. Pamoja na kuipa familia yake kipaumbele kuliko jambo lolote lile, anajivunia mabadiliko ya tija ambayo yeye na wenzake wameyaleta katika sekta ya ufugaji nyuki ndani ya nchi yake.

Muongo mmoja tangu kuingia kwenye biashara ya nyuki, anaona wanawake, akiwemo yeye mwenyewe, hawanyanyapaliwi tena, na kwa ujumla watu wanawaheshimu wafugaji nyuki na nyuki wenyewe pia.

Safari ya ujasiriamali ya Déborah imemfanya atambuliwe na taasisi za fedha, ikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Chini ya uongozi wake, Grecom imefanikiwa kutoa ajira kwa watu, kuanzisha chama cha ushirika kwa wafugaji nyuki, na mipango ya kuanzisha kituo cha utafiti kitakachoangazia nyuki na ufugaji nyuki kama shughuli za kusaidia uchumi.

Ukakamavu licha ya kuwepo vurugu

Juhudi na ndoto zote za Déborah karibu zitatizwe, wiki moja kabla ya TRT Afrika kumhoji, vikosi vya M23 na washirika wake walidhibiti mji wa Goma.

Kama ilivyokuwa kwa wakazi wengi, Déborah pia alikosa huduma ya maji, umeme na intaneti kwa majuma kadhaa.

Sehemu zake za biashara ziliharibiwa wakati wa vita pamoja na kuporwa.

Licha ya haya yote, ukakamavu wa Déborah ulimsaidia katika kuendelea na biashara yake.

Ana imani kuwa mustakabali wa mji wake na nchi yake utakuwa mzuri, akiwa na matumaini ya kuendeleza juhudi zake za kuimarisha sekta ya ufugaji nyuki nchini DRC.

TRT Afrika