Benki ya Zirat Katilim ya Uturuki imefungua tawi nchini Somalia, na kuwa benki ya kwanza ya kigeni kufanya kazi nchini humo baada ya zaidi ya miaka 50.
Hafla ya ufunguzi rasmi wa kihistoria wa Benki ya Ziraat Katilim ya Uturuki ilifanyika mwishoni mwa juma katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu huku sherehe hiyo ikihudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu kutoka mataifa hayo mawili.
Waziri wa Fedha wa Somalia Bihi Egeh, Meneja Mkuu wa Benki ya Ziraat Katilim ya Uturuki Metin Özdemir, Gavana wa Benki Kuu ya Somalia Abdirahman Mohamed Abdullahi, na Balozi wa Uturuki nchini Somalia, Ibrahim M. Yagli ni baadhi ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo ya ufunguzi.
Hatua hiyo imefanikiwa baada ya Benki hiyo ya Zirat Katilim kukamilisha vigezo vyote vya benki ya kigeni kuwekeza nchini Somalia na hatimae kukabidhiwa leseni na bodi ya wakurugenzi ya Benki Kuu ya Somalia mnamo mwaka jana.
"Huu ni ushindi wa kihistoria kwa watu wote wa Somalia, kwa benki ya Ziraat Katilim, kuwa benki ya kwanza ya kigeni kufanya kazi nchini kwa zaidi ya miaka 50," alisema Gavana wa Benki Kuu ya Somalia.
Hatua ya Benki ya kimataifa kufungua ofisi nchini Somalia, ni ishara ya maendeleo yaliyotekelezwa kwa mujibu wa sheria na ujenzi wa mfumo wa kifedha wa nchi, ambayo itaongeza imani ya wawekezaji wa kimataifa
Nae Waziri wa Fedha wa Somalia Bihi Egeh, amesifia kuwa biashara ya Somalia itafaidika kutokana na uwekezaji huo utakaounganisha ulimwenguni na kukuza uchumi wa nchi hiyo ambayo kwa miongo kadhaa imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya usalama.
Meneja Mkuu wa Benki ya Ziraat Katilim ya Uturuki Metin Özdemir, ameandika katika mtandao wa X, "Nalitakia tawi hili letu ambalo litakuwa daraja la kifedha kati ya Uturuki na Somalia kila la heri."
Hapo awali, Metin alifafanua kuwa ufunguzi wa tawi la benki hiyo utachangia pakubwa kuendeleza zaidi uhusiano na undugu wa kihistoria kati ya Somalia na Uturuki.
"Tunaenda huko kufanya kazi kwa upendo, undugu na uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Uturuki na Somalia, na tunalenga kuendeleza zaidi uhusiano wetu. Pia, tunawekeza kwa lengo la kufufua na kuendeleza biashara ya nje kati ya nchi zetu, " Alisema Metin.
Ziraat Katılım ni benki inayomilikiwa na serikali ya Uturuki, inahudumu katika nchi 20 tofauti, ikiwa na benki 15 na matawi 27 ulimwenguni kote.