Uturuki na Uingereza kupanua upeo wa makubaliano ya biashara huria, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amesema baada ya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na mwenzake wa Uingereza James Cleverly mjini Ankara.
"Tunakaribia kukamilisha maandalizi yetu," alisema, na kuongeza kuwa lengo ni kubadilisha kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kilichofikia takriban dola bilioni 20 mnamo 2022. Mkataba wa sasa wa biashara ulisainiwa mwezi Disemba 2020.
Bwana Fidan aliongeza kuwa, wawili hao pia walijadili masuala ya kikanda na kimataifa, ikiwemo pamoja na vita vinavyoendelea vya Ukraine, kurejeshwa kwa 'Mpango wa Nafaka ya Bahari Nyeusi' na mzozo wa Syria.
Mradi wa barabara ya maendeleo
Fidan amesema kuwa Uturuki, Iraq, Falme za Kiarabu na Qatar wanaendelea kujadiliana juu ya mradi wa barabara ya maendeleo ya Uturuki na Iraq.
Pia amekiri kwamba mabadiliko ya hivi karibuni ya kijiografia kama janga la UVIKO-19, mzozo wa Urusi na Ukraine na ushindani kati ya Marekani na Uchina yamezalisha umuhimu zaidi wa ubunifu wa njia mpya za biashara.
Kuhusu makubaliano ya kiuchumi kati ya India, Mashariki ya Kati na Ulaya yaliosainiwa katika mkutano wa G-20 uliokwisha wiki iliyopita New Delhi, Fidan alisema "wataalam wametilia shaka "ufanisi wake".
"Inaonekana kwamba wasiwasi wa kijiografia una jukumu muhimu," aliongeza.
"Kuna barabara nyingine ya kiuchumi ambayo iliibuka katika ajenda za mikutano ya G-20, na ombi lilipitishwa. Ni mradi wa barabara ya maendeleo ambao utaanza kutoka Ghuba ya Basra, ukipitia Iraq na kuishia nchini humo.
"Kwa sasa Uturuki ina shughulika zaidi na mradi huu. Hasa Iraq, UAE, Uturuki na Qatar wanaohusika katika majadiliano zaidi juu ya suala hili."
Waziri Fidan alisema Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, haswa katika mkutano wake na Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu UAE Mohammed bin Zayed Al Nahyan, alikubali kwamba makaratasi rasmi juu ya mradi huo yanapaswa kukamilika na kutekelezwa ndani ya miezi michache ijayo.
Mgogoro wa Sudan, mafuriko nchini Libya
Katika kujibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari, Waziri Fidan pia alitoa jibu kuhusu swali lililogusia mkutano kati ya Rais Erdogan na Abdel Fattah al-Burhan wa Sudan mjini Ankara. Fidan alisema kuwa viongozi hao walizungumzia majadiliano ya amani yanayoendelea na utoaji wa misaada ya kutatua shida za kibinadamu na kiuchumi zinazoendelea.
"Rais wetu alisisitiza dhamira yetu ya kutoa kila aina ya msaada kwa Sudan. Ilisisitizwa kuwa ikiwa kuna huduma yoyote tunaweza kutoa ili kufanikisha amani, tuko tayari muda wowote, " Mwanadiplomasia huyo wa Uturuki alisema.
Fidan pia alitoa salamu zake za rambirambi kwa Libya ambayo imekumbwa na mafuriko mwanzoni mwa juma, huku akisema Uturuki imetuma msaada na itaendelea kufanya hivyo kutokana na mahitaji ya kibinaadam.