Bidhaa za Uturuki Tanzania

Na Lulu A. Sanga

Si jambo la kushangaza kusikia “mapazia kutoka Uturuki, kapeti za Uturuki, nguo za watoto kutoka Uturuki.” Haya utakuta kwenye masoko makubwa Tanzania kama vile Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha na hata kupitia mitandao ya kijamii.

Wauzaji husisitiza kwamba “hii bidhaa ya Uturuki” lengo ni kuaminisha kuwa ni bidhaa yenye ubora na hata gharama yake haiwezi fanana na bidhaa nyengine.

Bidhaa nyingi zaidi huingizwa kutoka China, lakini kwa miaka ya hivi karibuni imeshuhudia wimbi kubwa la wafanyabiashara wa Tanzania wakienda kufuata mizigo Uturuki ili kuingiza Tanzania.

TRT Afrika imezungumza na Bahati Mwanjala ambae ni mfanyabiashara wa Tanzania anayechukua bidhaa zake Uturuki na China. Anasema Uturuki wanavitu vizuri na bora hawawezi kufanana na China na hata watumiaji wenyewe wanajua na wanaelewa hilo, changamoto kubwa tu ni kwamba Uturuki si wabunifu sana.

“Kwa ubora tu vitu vya Uturuki ni imara sana na kwa watumiaji au wateja wetu wao wanafahamu sema inategemea na kipato kwa wale wenye hela hawajali kuhusu gharama wao watanunua mali ya Uturuki tu, lakini kwa wale wa kipato cha chini wao wananunua bidhaa za China kulingana na kipato,” anaongeza Bahati.

Baadhi ya maduka hupewa jina la Uturuki

Lakini je ni kweli kuna tofauti kati ya bidhaa za Uturuki na zile zinazotoka nchi nyingine?

TRT Afrika imezungumza na Christian Kivengi mtumiaji wa bidha hizo, anasea yupo tayari kutoa pesa yake hata kama ni nyingi ilimradi apate kitu bora na kinacho dumu.

“Hizi nguo za ndani tunanunua moja kwa shilingi elfu kumi lakini unatumia mpaka moyo unatulia nguo haitepeti na wala haikusanyi jasho, huwezi fananisha hii ya Uturuki na zile za nchi nyengine, hata ukitazama kwa macho na kuzishika utagundua utofauti.”

Kama biashara inaenda na upepo basi upepo wa sasa hivi unaonekana kuelekewa Uturuki. Watu wengi wanaamini vitu vya nchi hiyo ni bora na ni vya asili, hakuna bidhaa ya kughushi.

“Kitu cha Uturuki kikitoka kimetoka kikiisha kimeisha yaani kwa ubora ni bora kwa mfano viatu nguo ni bora zaidi. Bidhaa zinachukua muda mrefu kufika ila zinadumu sana,” anasema Bertha Robert muuzaji na mtumiaji wa bidhaa kutoka Uturuki.

Nae, mkufunzi wa maswala ya biashara na masoko Tanzania Kelvin Kibenje anasema Tanzania hakuna viwanda vya kutosha vinavyoweza kukidhi mahitaji ya soko hali inayopelekea wananchi wengi wanaofanya biashara kufwata bidhaa nje ya nchi hasa bara la Asia na Ulaya.

Majina ya maduka mengi utakuta yameandikwa Uturuki huku kupitia mitandao ya kijamii imewekwa wazi zaidi kwa kuwa na kurasa hasa za mtandao wa Instagram zikionyesha ama kutangaza bidhaa kutoka Uturuki.

Bidhaa za uturuki huuzwa kwa gharama na watu bado huzimaliza

Kwa upande wa wafanya biashara wanaouza mali hasa nguo hapa Uturuki wao wanasema ubora ni muhimu zaidi kwa bidhaa zinazo toka katika nchi yao kuliko kitu chochote.

"Uturuki si nguo pekee kila kinachotoka hapa kinatengenezwa kwa umakini na ubora zaidi. Bidhaa zinabeba jina la nchi" anasisitiza Salman muuzaji wa nguo Aksaray Ururuki.

Lakini swali langu bado lipo palepale, je Uturuki ndio jina jipya linalo maanisha ubora Tanzania?

TRT Afrika