Facebook - Meta / Photo: AA

Juhudi za mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) za kubuni vyanzo vipya vya kukusanya mapato ili kupanua wigo wa kodi nchini humo zinaonekana kufanikiwa baada ya Meta kutangaza utozaji ushuru wa ongezeko la thamani (VAT) kuanzia tarehe 1 Desemba 2023 kwenye matangazo ya Facebook (Ads).

Kampuni kubwa ya mitandao ya kijamii ya Kimarekani Meta, inayomiliki mitandao ya Facebook, Instagram na WhatsApp, kutoa taarifa kuwa matangazo ya Facebook nchini Tanzania yataanza kutozwa ushuru wa ongezeko la thamani (VAT) wa 18%.”

Tanzania inafuata nyayo ya nchi jirani ya Kenya ambayo ilianza kutoza ushuru wa ongezeko la thamani (VAT) 16% kwenye matangazo ya Facebook kuanzia Novemba 1, 2022.

Nchi nyingine za kiafrika zilizoanza kutoza kodi ya huduma za dijitali ni pamoja na Nigeria na Afrika Kusini.

“Kuanzia tarehe 1 Desemba 2023, matangazo ya Facebook nchini Tanzania yanatozwa ushuru wa ongezeko la thamani (VAT) wa 18%.”

Mnamo mwezi Aprili mwaka 2022, wawakilishi wa kampuni ya Meta na maafisa wa TRA Tanzania walifanya mazungumzo ya awali mjini Dar es Salaam.

Walijadili jinsi ya kutoza kodi huduma tofauti nchini humo.

Maafisa wa TRA wakiwa mkutanoni na wataalam wa Meta jijini Dar es Salaam. Picha: TRA Tanzania

Takwimu zilizochapishwa na mtandao wa Meta mwanzoni mwa 2022, zilionyesha kuwa watumiaji wa Facebook nchini Tanzania ilikuwa zaidi ya milioni 4.

TRT Afrika