Vikosi vya usalama kutoka Rwanda vikiwa kwenye lindo katika mji wa Palma katika kukabiliana na wanamgambo. /Picha: Reuters

Siku ya Jumamosil, waendesha mashitaka wa Ufaransa wamesema kuwa wanaichunguza kampuni ya mafuta ya TotalEnergies kwa kuhusika na mashambulizi ya kigaidi ya mwaka 2021, yalioua mamia ya watu nchini Msumbiji.

Uchunguzi huo unafuatia malalamiko kutoka kwa familia za waathirika na manusura wa tukio hilo, wakiituhumu kampuni hiyo kwa kushindwa kuwalinda wakandarasi wake, waendesha mashitaka hao wameiambia AFP.

Manusura na familia zao wanasema kuwa TotalEnergies pia ilishindwa kutoa mafuta ili helikopta ziweze kuwahamisha raia baada ya wanamgambo kuua makumi ya watu katika mji wa bandari wa Palma nchini Msumbiji mnamo Machi 24, 2021.

Shambulizi hilo katika jimbo la Cabo Delgado lilidumu kwa siku kadhaa, na kusababisha vifo vya mamia ya watu huku baadhi ya waathirika wakikatwa vichwa na wengine kuyakimbia makazi yao.

Kukosekana kwa msaada

Msemaji wa TotalEnergies, ambaye alitafutwa na AFP kwa mahojiano zaidi sku ya Jumamosi, alisisitiza kuwa kampuni hiyo "inakataa kwa uthabiti shutuma hizo"

Alisema kuwa kampuni hiyo, kwa upande wa Msumbiji ilitoa msaada wa dharura na kuwezesha kuwahamisha watu 2,500 kutoka kwenye mtambo huo, wakiwemo raia, wafanyakazi, wakandarasi na wengineo.

Jopo la uchunguzi kutoka Ufaransa pia unatafuta kubaini ikiwa TotalEnergies ina hatia ya kutowasaidia watu walio katika hatari, waendesha mashtaka walisema.

Walalamikaji saba wa Uingereza na Afrika Kusini - watatu walionusurika na jamaa wanne wa waathirika - wanaishutumu TotalEnergies kwa kushindwa kuchukua hatua kuhakikisha usalama wa wakandarasi kabla ya shambulizi hilo.

Ngome ya wanamgambo

Kundi la Al-Shabab, ambalo halina uhusiano na kundi la Kisomali, lilitekeleza shambulio hilo, baada ya kuwepo katika eneo hilo toka 2017 na kukaribia zaidi Palma.

"Hatari ilijulikana," alisema wakili wa walalamishi Henri Thulliez mwaka 2023 wakati wa kesi hiyo.

Kulingana na matokeo ya uchunguzi wa awali, kesi hiyo ingetupiliwa mbali, au upelelezi utazidishwa kwa nia ya kuleta mashtaka, walisema.

Familia na walionusurika walifurahia uamuzi wa Ufaransa, huku Nicholas Alexander, manusura wa shambulio la Afrika Kusini, akiuita "hatua nzuri".

TotalEnergies, alisema, ilibeba "sehemu ya jukumu" katika mkasa huo, aliiambia AFP.

Anabela Lemos, mwanaharakati katika shirika la 'Marafiki wa Dunia' nchini Msumbiji, anayejulikana kama Justica Ambiental -- alisema "athari mbaya" za oparesheni za mafuta zilichochea "uharibifu" wa mazingira na "vifo".

Kusimamishwa kwa mradi

Mradi wa TotalEnergies wa dola bilioni 20 wa gesi katika peninsula ya Afungi ulisitishwa kufuatia shambulio la 2021, licha ya mwenyekiti Patrick Pouyanne, kuonesha matumaini ya kuufufua.

Mnamo Novemba 2023, mashirika yasiyo ya kiserikali 124 yalichapisha barua ya wazi kwa taasisi nyingi za kifedha, zikiwemo benki za Ulaya, Japan na Afrika Kusini, zikizitaka kujiondoa kwenye mradi huo.

Mradi huo ulitishia mifumo ya ikolojia ya ndani na hali ya hewa ya kimataifa, huku ukishindwa kunufaisha jamii za wenyeji, walisema.

Msumbiji imeweka matumaini makubwa katika hifadhi kubwa za gesi asilia - kubwa zaidi kupatikana kusini mwa Sahara - ambazo ziligunduliwa katika jimbo hilo la kaskazini mwaka 2010.

AFP