Kenya imepata bei ya juu kiasi ya mafuta katika miezi ya hivi majuzi katika ukanda wa Afrika Mashariki. / Picha: AP

Bei za mafuta nchini Kenya zimeshuka katika mapitio ya hivi karibuni yaliyofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli ya Kenya (EPRA).

Lita moja ya petroli imepungua kwa shilingi 5 za Kenya ($0.03), dizeli Ksh2 ($0.01), na mafuta ya taa Ksh4.0 ($0.03).

Katika mji mkuu wa Nairobi, lita moja ya petroli itauzwa kwa Ksh212.36 ($1.38), dizeli Ksh201.47 ($1.31) na mafuta ya taa Ksh199.05 ($1.30).

Bei za mafuta katika miji mingine mikubwa ya Kenya kama Kisumu, Nakuru na Eldoret zinafanana karibu na bei za Nairobi.

Kushuka kwa Bei za Kimataifa

Katika jiji la bandari la Mombasa, ambapo mafuta yanatua baada ya kuagizwa, lita moja ya petroli itauzwa kwa Ksh209.3 ($1.36), dizeli Ksh198.41 ($1.29) na mafuta ya taa Ksh195.92 ($1.28).

"Kiwango cha wastani cha gharama ya uagizaji wa petroli kimepungua kwa 16.11% kutoka $827.75 kwa kila mita ya ujazo mnamo Oktoba 2023 hadi $694.44 kwa kila mita ya ujazo mnamo Novemba 2023; dizeli imepungua kwa 5.43% kutoka $873.42 kwa kila mita ya ujazo hadi $826.01 kwa kila mita ya ujazo huku mafuta ya taa yakipungua kwa 6.63% kutoka $813.90 kwa kila mita ya ujazo hadi $759.93 kwa kila mita ya ujazo," EPRA ilisema katika taarifa yake siku ya Alhamisi.

Bei hizi zitabaki kama zilivyo kati ya Desemba 15 na Januari 14, 2024.

Taifa hili la Afrika Mashariki limekuwa na ongezeko kubwa la bei za mafuta katika miezi ya hivi karibuni. Mapitio haya ya hivi karibuni ya kupunguza bei yanakuja kama ahueni kwa wengi kabla ya sherehe za mwisho wa mwaka.

TRT Afrika