Wabunge nchini Uganda wametilia shaka ubora wa elimu wanayopata wanafunzi nchini humo katika vyuo vya elimu ya juu na vya chini.
Hii ni baada ya ripoti kubaini kuwa baadhi ya vyuo vikuu vya umma vina walimu asilimia 12 pekee ya wanaohitajika.
Hii ni baada ya Waziri wa Elimu ya Juu, Moriku Kaducu kutetea uamuzi wa Chuo Kikuu cha Kyambogo kuwafuta kazi baadhi ya watumishi wa muda kabla ya Mwaka wa Masomo 2024/2025.
Waziri amedai walimu hao wa muda waliajiriwa tu na wakuu wa idara ambao waliwasilisha majina yao kwa ajili ya uteuzi, lakini mabadiliko ya sera yaliimarisha mchakato wa kuajiri, na wale wasio na sifa za kutosha walipunguzwa kazi ili kushughulikia viwango vya chini vya asilimia 30 ya wafanyakazi wa kufundisha.
“Tunazungumza kuhusu Chuo Kikuu cha Kyambogo, lakini tatizo hili liko katika Vyuo Vikuu vyote na sidhani kama kuna wakati mwingine tutazungumza kuhusu Chuo Kikuu cha Muni, Chuo Kikuu cha Gulu, nafikiri tuzungumzie sasa vyuo vikuu vyote hivi," Emmanuel Ongiertho mbunge wa Kaunti ya Jonam alibainisha.
"Unapata asilimia 30 ya walimu katika Chuo Kikuu cha Kyambogo ni bora zaidi kuliko Vyuo Vikuu vyengine. Hasa wale wapya wana asilimia 25 tu ya walimu," Ongiertho alisema.
"Walakini, ikiwa vyuo vikuu viko hivyo, ni vibaya zaidi katika vituo vya chini vya elimu kuanzia shule za msingi, unakuta walimu saba katika shule nzima. Ni lazima tuwe na dhamira ya kuona kwamba utumishi wa taasisi zote unashughulikiwa ili tuzungumzie elimu bora katika taifa hili," Connie Nakayenze mwakilishi wa wanawake katika mji wa Mbale amesema.
"Ni lazima tukumbuke kuwa walimu wa muda ndio wanaoshikilia vyuo vikuu hivi. Wao ndio wanaofanya kazi kubwa na ikiwa hawajalipwa, inasikitisha sana," Nakayenze ameongezea.
"Tunatakiwa kuwekeza kwenye elimu, tuseme na kutenda. Wafanyakazi wa muda wa kufundisha, kwanza kabisa, tuwalipe tunachodai kabla hatujawafukuza. Kwa bahati mbaya, wanaweza kwenda mahakamani na kisha, utahitajika kuwalipa hata zaidi," Joel Ssenyonyi, kiongozi wa upinzani bungeni amesisitiza.
"Tulichonacho sasa ni elimu ya wingi, kinyume na elimu bora. Tuna wanafunzi wengi, lakini ni aina gani ya elimu wanayopata?" Ssenyonyi aliuliza wabunge wenzake.
Wabunge wengine wamesema changamoto hii inatokana na mipango mibovu katika sekta mzima ya elimu.
"Ukiangalia elimu, kuanzia ngazi ya msingi, kuna shule za msingi zenye walimu sita tu kwenye orodha ya malipo ya serikali. Kuna shule za sekondari ambapo unakuta walimu 8-9 kwenye orodha ya malipo ya serikali badala ya walimu 20-30. Nadhani tunatakiwa kuwa kuchukulia uzito masuala haya. Je, tunapanga nini?" Kahonda Donozio mbunge wa Ruhinda Kusini alisema.