Wabunge nchini Uganda wamemtaka Waziri wa Kilimo, Viwanda vya Wanyama na Uvuvi, kuharakisha utekelezaji wa Sheria ya Uvuvi na Ufugaji wa Samaki ya mwaka 2022 kama njia ya kudhibiti matumizi ya zana duni za uvuvi.
Suala hili liliibuka katika majadiliano bungeni Jumatano, 31 Januari 2024.
Walisema sheria hiyo, iwapo itatekelezwa, pia itaepusha madai ya mara kwa mara ya ukiukaji wa haki za binadamu kwa wavuvi unaofanywa na watendaji wa usalama.
Bunge lilipitisha Sheria hiyo mwezi Februari, 2022 lengo lake miongoni mwa mengine; ni kutoa leseni, na udhibiti wa shughuli za uzalishaji wa uvuvi na ufugaji wa samaki, mbinu za uvuvi na zana zake.
Mnamo mwaka wa 2017, Rais Yoweri Museveni alliiagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) kupelekwa kwenye eneo la maziwa ya Uganda ili kukabiliana na vitendo vya uvuvi haramu ili kulinda rasilimali ya samaki ambayo ilikuwa katika tishio la kupungua.
Agnes Atim mwakilishi wa wanawake kutoka wilaya ya Amolatar kaskazini mwa Uganda, amedai kuwa kutokana na kukosekana kwa kanuni, wavuvi wanadanganywa na kuteswa na wanajeshi wa UPDF kwa madai ya kutumia zana duni za uvuvi kutoka nje ya nchi.
"Kuna haja ya kuchunguza, kukamata, kuandamana na kuwashtaki wafanyabiashara hawa haramu wa nyavu na kuwasaidia wavuvi kwa kuwapa nyavu halali za uvuvi, boti na injini. Wavuvi wa nchi hii hawajawahi kuhudumiwa, kile wanachopokea ni kifo,” alisema.
Naye Peter Okeyoh, mbunge wa Bukooli alisema kuwa wavuvi wanalazimika kununua zana za uvuvi zilizoagizwa kutoka nje kwa gharama ya juu, na hivyo kuathiri biashara zao.
“Ni maombi yetu kwamba tuangalie masaibu ya wavuvi. Haki zao zinadhulumiwa,” aliliambia bunge.
Abed Bwanika mbunge wa Kimaanya-Kabonera amelaumu vitendo hivyo kwa kutokuwepo kwa kanuni za kutekeleza Sheria ya Uvuvi na Ufugaji wa samaki.
“Kwa kuwa tulipitisha sheria hiyo, hakuna kanuni na ndiyo maana hata UPDF haiwezi kuondoka katika maeneo ya uvuvi. Lazima kuwe na sheria inayotekelezwa,” alisema.
Wabunge wengine wametaka kupigwa marufuku kwa nyavu, na hata nyuzi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
Naibu Spika, Thomas Tayebwa, amempa mwezi mmoja Waziri wa Kilimo ambaye hakuwepo bungeni kuwasilisha kanuni hizo.