Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesema "natumai serikali ya Marekani itafikiria upya uamuzi wake wa kujiondoa katika Shirika la Afya Duniani, WHO."
Rais wa Marekani Donald Trump baada ya kuapishwa Januari 20, 2025, alitia saini amri ya kuiondoa Marekani katika uanachama wa Shirika la Afya Duniani, WHO.
Rais Trump amedai kuwa Shirika hilo linachukua fedha nyingi za Marekani ilhali halitimizi majukumu yake.
Umoja wa Afrika unaitambua Marekani kama mwanachama mwanzilishi wa Shirika hilo la afya.
"Marekani kama mwanachama wa WHO, ilikuwa muhimu katika kuunda vyombo na kanuni za kimataifa za WHO kuhusu usalama wa afya ya umma na ustawi katika miongo saba iliyopita," Faki amesema katika taarifa.
"Leo, zaidi ya hapo awali, ulimwengu unategemea WHO kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha usalama wa afya ya umma kama faida ya pamoja. Kwa hiyo, Mwenyekiti anatumai kuwa serikali ya Marekani itafikiria upya uamuzi wake wa kujiondoa katika Jumuiya hii muhimu ya kimataifa ambayo ni mwanachama mwanzilishi," taarifa hiyo imesema.
Faki amesema Marekani ilikuwa msitari wa mbele wakati wa kuundwa kwa Shirika la Afya la Afrika, Africa CDC ambalo linafanya kazi na WHO.