Wabunge Uganda wapitisha mswada wa kuongeza siku za likizo ya uzazi kwa wanaume

Wabunge Uganda wapitisha mswada wa kuongeza siku za likizo ya uzazi kwa wanaume

Muswada huo ulifadhiliwa na serikali na wabunge walisema wanachukua mfano huo kutoka nchi jirani za Tanzania na Kenya
Bunge la taifa Uganda  / Photo: Reuters

Bunge la Uganda limepitisha mswada uliopendekeza kuongeza likizo ya kulipwa ya uzazi kutoka siku nne hadi saba ili kuruhusu wafanyakazi wa kiume kutoa msaada kwa wenzi wao.

"Tunatamani kuwa na jamii ambayo wanaume watakuwa na jukumu kubwa la kusaidia wazazi wenzao wa kike, ni muhimu muda zaidi utolewe kwa wafanyakazi wa kiume kuwasaidia wake wao," Flavia Kabahenda, mwenyekiti wa kamati ya jinsia ya bunge, alinukuliwa akisema bungeni.

Mswada huo ulifadhiliwa na serikali na wabunge walisema wanachukua mkondo huo kutoka nchi jirani za Tanzania na Kenya ambapo wafanyakazi wa kiume wanapewa siku tano na 14 mtawalia za likizo ya uzazi yenye malipo.

Bunge la Uganda hata hivyo lilitupilia mbali pendekezo la kuongeza likizo ya uzazi kutoka siku 60 hadi 90 kwa wafanyikazi wa kike walio na watoto wengi.

Mwanasheria Mkuu Kiryowa Kiwanuka anaripotiwa kusema itakuwa dhuluma kwa waajiri.

Mswada huo sasa unasubiri idhini ya Rais Yoweri Museveni kabla ya kuwa sheria.

TRT Afrika