Waziri Mkuu wa Uganda Robinah Nabbanja amewataka wabunge wa upande ya upinzani kuwasilisha michango yao kwa wananchi walioathirika na maafa ya dampo katika eneo la Kiteezi, jijini Kampala.
Mnamo tarehe 9 Agosti 2024, mvua kubwa ilisababisha maporomoko ya ardhi katika eneo la kutupia taka katika eneo la Kiteezi huko Kampala, Uganda, na kuua takriban watu 21.
Waziri Mkuu huyo, alitoa kauli hiyo wakati akijibu hoja iliyotolewa na kiongozi wa kambi ya upinzani, Joel Ssenyonyi ambaye alimtaka Waziri Mkuu kufafanua jinsi waathirika ambao nyumba zao zilifukiwa na vifusi vya takataka na kwa sasa, wamepata hifadhi chini ya mahema.
" Ninasema, dola 520 ni kitu kidogo kwa watu waliopoteza kila kitu. Sijui ulikujaje na hesabu hii. Labda kama tunaweza kuwa na uelewa mzuri zaidi kwa sababu sisi tunaotangamana na watu hawa na mahitaji yao ya dharura, dola 520 ni pesa ndogo kwa kweli," alisema Ssenyonyi.
“Mstahiki Meya, Elias Lukwago na viongozi wengine wengi akiwemo mbunge wa eneo hilo, Muwadda Nkunyingi walikuwa kwenye mkutano huo tulipofanya uamuzi huo kwa nia njema. Ni vyema kila mtu apate mahali pa kukodisha na kuwaondoa mahali hapo," Nabbanja aliliambia bunge la nchi hiyo.
"Wewe kama kiongozi wa kambi unaweza kutoa mchango fulani kwani watu wamekuwa wakichangia,” aliongeza.
“Moja ya mambo ya kusumbua niliyoyaona ni kwamba watu hawa wameingizwa kwenye mahema madogo matatu, mahema haya yana joto kali sana. Waliniuliza, mwenyekiti, unaweza kuingia mwenyewe ujionee . Bila shaka nisingeweza,” alieleza Alex Byarugaba, mbunge kutoka eneo la Kusini la Isiringo.
"Wanawake wanakaa peke yao, wanaume wanakaa kwenye hema jingine. Nilidhani kuwa, kabla hatujafanya yote hayo, hatuwezi kupata japo mahema 230 kutoka kwa serikali ili kila familia iwe na hema lake?" alihoji mbunge huyo.
Hata hivyo, pendekezo lake lilikataliwa na Waziri Mkuu Nabbanja na Spika wa Bunge hilo, ambapo walisisitiza haja ya wakazi hao kupokea fidia ya dola 520 na kuondoka kwenye mahema hayo, ili kutoa nafasi ya kucheza kwa wanafunzi wa shule ya msingi Kiteezi.