Kiongozi wa Upinzani bungeni, nchini Uganda, Joel Ssenyonyi amewataka viongozi wazee serikalini kuifahamu vyema lugha ya Gen Z akidai kuwa wanaongoza taifa ambalo lina idadi kubwa ya vijana.
Matamshi haya aliyasema bungeni baada malalamiko yaliyotolewa na Waziri wa Serikali ya Mtaa, Raphael Magyezi akimtuhumu Ssenyonyi kutumia matamshi makali aliposema Waziri huyo ni “Mwendawazimu,” akitumia jina "mad" kwa Kiingereza.
“Kiongozi wa upinzani wakati anasoma maelezo yake alisoma taarifa fulani ambayo sikukubaliana nayo na nadhani aliniona nikitikisa kichwa akasema, 'naona Magyezi ako mad," alisema Magyezi.
Magyezi alidai maelezo hayo yanapakana na kuhoji afya yake ya akili, na alimtaka Naibu Spika, Tayebwa ahakikishe maneno hayo yanafutwa kwenye rekodi ya Bunge, ili yasiwachanganye wasomaji wajao wa Hansard kwamba Waziri wakati huo alikuwa mgonjwa wa akili.
Joel Ssenyonyi alikuwa akiongelea hotuba ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
"Wakati nchi inazama, hatuwezi tu kuwa watazamaji ili kuwashangilia wale wanaoiongoza nchi yetu kukamilisha uharibifu, lakini tunapiga hatua mbele kuvumilia. Mapambano ya dhati ya kuikomboa nchi yetu kutoka kwa wale wanaotumia madaraka bila kuwajibika na kinyume na matakwa na matarajio ya raia.”
Na hapo ndipo alitumia jina" mad"
“Taarifa yangu iliainisha wazi maeneo ambayo yanazama ambayo sote tunapaswa kuyashikilia, ambayo sote lazima tuyafanyie kazi kwa manufaa yetu sote. Niliposema namuona Magyezi ni “mad”, neno "mad" lina maana nyingi ikiwemo hasira, niliona umekasirika," Ssenyonyi alijitetea.
"Ndivyo nilivyomaanisha kwa sababu simfahamu Magyezi kwa kuwa na kichaa kwa maana ya kuwa mgonjwa wa akili. Unaona, Gen Z wanajua maneno haya mapya ya Kiingereza, kwa hivyo mwenzetu mkuu anahitaji kujifunza maneno hayo. Lakini kwa uwazi, sikumaanisha kuwa umechanganyikiwa kiakili kwa sababu sidhani kama umechanganyikiwa, nilimaanisha kuwa ulikuwa na hasira,” alisema Ssenyonyi.