Na Kudra Maliro
Watu wa asili wanajulikana kwa mitindo yao ya kipekee ya maisha, lugha tofauti na tamaduni mbalimbali, takriban jumuiya elfu tano za Wenyeji kote ulimwenguni zinakabiliwa na vitisho vingi katika ulimwengu unaoendelea kwa kasi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) linasema kuwa kwa miongo kadhaa, watu wa kiasili wamekuwa wakitaka kutambuliwa kwa asili yao maeneo na maliasili zao, lakini wanaendelea kuteseka kwa ubaguzi na dhuluma.
Siku ya watu wa Kiasili
Siku ya Watu wa Kiasili “huadhimishwa kila mwaka tarehe 9 Agosti, Siku ya Kimataifa ya Watu wa Asili Duniani ni fursa ya kuenzi jamii hizi na ujuzi wao,” alisema Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku hiyo.
Watu wa kiasili wanawakilisha watu milioni 476 katika nchi 90. Ingawa wanachukua 5% tu ya idadi ya watu ulimwenguni, kwa sasa ni 15% ya watu waliotengwa zaidi kwenye sayari.
"Katika Siku ya Wenyeji, tunasherehekea vijana wa kiasili na jukumu lao katika kuleta mabadiliko. Ni lazima wahusishwe katika maamuzi yanayoathiri maisha yao ya baadaye," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alichapisha kwenye X iliyojulikana kama Twitter siku ya Jumatano.
Kuna takriban watu 10,000 wa kiasili ya Batwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambao tayari wamepoteza njia halali ya kuingia katika nchi yao, ambayo imegeuzwa kuwa eneo la uhifadhi wa sokwe walio hatarini kutoweka.
Wanasubiri kwa hamu ahadi kutoka kwa mamlaka ili warudi kwenye maisha ya heshima.
Chini ya mada "Vijana wa kiasili kama mawakala wa mabadiliko ya kujitawala", watu wa kiasili wanatafuta kutambuliwa kwa haki zao na kukuza urithi wao.
Nchini DRC. sheria 22/030 la tarehe 15 Julai 2022 kuhusu ulinzi na uendelezaji wa haki za watu wa kiasili wa mbilikimo ilitangazwa.
Sheria hii inakomesha kutengwa na ubaguzi unaoteseka na watu wa kiasili wa mbilikimo. Inawapa ufikiaji wa bure wa elimu, haki na utangazaji wa bidhaa za asili za dawa.
Hakuna kilichobadilika
Kwa jamii ya Batwa, hata hivyo, hakuna kilichobadilika.
Wakiwa wamehamishwa na mamlaka kutoka Hifadhi ya Kitaifa ya Kahuzi-Biega katika miaka ya 1970, Wabatwa sasa wanatishia kurudi kwenye msitu ambao wanadai kuwa makazi yao halali.
Jean-Marie Kasula, rais wa jamii ya Mbilikimo (Batwa) katika kijiji cha Muyange, hafichi kusikitishwa kwake na kuchelewa kutekeleza ahadi zilizotolewa na serikali tangu 2019.
“Nina wasiwasi mkubwa kuona watu wetu wanakufa kwa njaa na maradhi bila kupata njia halali za kujikimu kimaisha au njia mbadala ambazo tumeahidiwa”, alisema Kasula.
Tofauti za kisimu na kitamaduni
Kulingana na UNESCO, watu wa kiasili wamerithi tofauti kubwa za lugha na kitamaduni, pamoja na mila na tamaduni za mababu.
Wana tamaduni zisizopungua 5,000 na huzungumza lugha nyingi kati ya 7,000 au zaidi za ulimwengu.
"Maarifa na mila asilia zinaweza kusaidia kutatua changamoto nyingi za leo," Bwana Guterres aliongeza.
Licha ya utofauti wao, watu wa kiasili wengi hushiriki mambo yanayofanana muhimu, hasa uhusiano wao na ardhi ya mababu zao na mazingira yao, pamoja na hamu ya kuhifadhi njia yao ya kujipanga na maadili yao ya kitamaduni, kijamii na kiuchumi, ambayo mara nyingi hutofautiana na kanuni kuu ya jamii wanapoishi.
Kila mwaka tarehe 9 Agosti, ulimwengu huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watu wa Kiasili Duniani ili kuhamasisha umma kuhusu haja ya kuheshimu haki za watu wa kiasili.
Tarehe hiyo ilichaguliwa kuadhimisha mkutano wa kwanza wa Kikundi Kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu Watu wa Kiasili, uliofanyika Geneva mwaka 1982.