Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres siku ya Jumanne, alisema kuwa 'anaumia moyo' kuona Waislamu wengi wa Gaza, Sudan na maeneo mengine wakishindwa kusherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr inayoashiria kumalizika kwa mfungo wa mwezi wa Ramadhan kwa sababu ya migogoro na njaa.
"Kila mwaka, huwa natoa salamu zangu za Eid al-Fitr kwa jumuiya yote ya Waislamu duniani kote," Guterres alisema kupitia ujumbe wake kwenye ukurasa wake wa X.
"Naumizwa moyo kuona Waislamu wengi wa Gaza, Sudan na sehemu nyinginezo watashindwa kusherehekea vizuri kutokana na njaa na migogoro," aliongeza.
Sudan imekumbwa na mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo na lile la Rapid Support Forces (RSF) tangu Aprili mwaka jana. Zaidi ya watu 13,000 wameuawa na zaidi ya milioni 8 wameyakimbia makazi yao kulingana na Umoja wa Mataifa, wakati nusu ya watu, au watu milioni 25, wanahitaji msaada wa kibinadamu.
Kwa upande mwingine, zaidi ya Wapalestina 33,000 wamepoteza maisha kufuatia uvamizi wa Israel wa Oktoba 7, 2023.
Sehemu kubwa ya miundombinu ya Gaza imeharibiwa vibaya kutokana na mashambulizi ya Israel, huku wakazi wake milioni 1.9 wakilazimika kuyahama makazi yao kutokana na hatari ya magonjwa na njaa.