Madaktari wanafunzi nchini Uganda. 

Waziri wa Afya wa Uganda Anifa Kawooya amelaumu uhaba wa rasilimali kama chanzo ha kushindwa kuwapeleka madaktari wanafunzi wote kwa ajili ya kupata mafunzo.

Amesema serikali haina uwezo wa kuajiri wataalamu au wasimamizi wengi katika hospitali na kufungua vituo vingi vya mafunzo kwa ajili ya kukabiliana na ongezeko la idadi ya wataalamu wakufunzi nchini.

Waziri huyo amesema jumla ya wahitimu madaktari 2,700 wanafaa kupewa nafasi katika vituo vya afya, kuongeza idadi ya madakitari 743 waliohitimu mafunzo ambao wanangoja kupewa nafasi.

"Wahitimu wa mwaka 2024 watatafutiwa nafasi katika siku zijazo wakiwemo wale waliokuwa wamepewa nafasi kwa makosa waliotoka Chuo Kikuu cha Christian University na Chuo Kikuu cha Makerere, wataondolewa pia kwa sasa," Kawoya alisema.

“Wahudumu wa afya wamepangwa katika vituo 73 vya mafunzo kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe 5 Agosti 2024 hadi Julai 31, 2025. Nafasi hii inahusisha wahitimu waliomaliza masomo yao mapema 2023 na kabla. Zaidi ya hayo, kipaumbele kimepewa kwa madaktari wa upasuaji, wa meno na wafamasia waliofadhiliwa na serikali tu wa kundi la 2024,” alisema Kawooya.

Suala hili limezua mjadala

Jesca Ababiku mbunge wa Adjumani aliiomba serikali kupunguza Shs1M ($269) zinazolipwa kwa kila mhudumu wa afya, kutokana na uhaba wa fedha, akisema kuwa hatua hiyo itahakikisha kuwa madaktari wanafunzi wengi wanasambazwa kulingana na rasilimali zilizopo, tofauti na kupeleka wachache tu.

"Pendekezo langu ni kuelewa jinsi takwimu hii ya Shs1M ($269) ilivyofikiwa, katika mazingira ambayo hatuna fedha za kutosha, ni afadhali tuangalie fedha hizi, tuzipange upya, kuliko kutopeleka baadhi ya watu," alisema Ababiku.

"Je, Wizara inaweza kushirikiana na pengine kutafuta bajeti ya ziada kwa sababu hatuna uwezo wa kuwaona hawa wanafunzi wataalamu wakizurura barabarani?" John Faith Magolo mbunge wa Bungokho Kaskazini aliuliza.

"Hatuwezi kuwa hapa na kuomboleza wakati suluhisho lazima litoke hapa, wanatafuta suluhisho," ameongezea.

Naibu Spika wa Bunge pia ameongezea kauli yake.

"Kuna baadhi ya wanafunzi madaktari kutoka nchi za nje hasa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wako pamoja chini ya Baraza la Madaktari la Afrika Mashariki na baadhi ya watu hawa wanachukua nafasi hapa nchini," Naibu Spika wa Bunge Thonmas Tayebwa ameelezea.

"Mwanafunzi anasema, 'Tafadhali, nahitaji kukamilisha elimu yangu. Niwezeshe kukidhi mahitaji yangu, mimi, ninapatikana, ni wewe unayehitaji kunisaidia, ikiwa hutafanya hivyo, unaweza hata kuiacha na kuniacha nifanye mazoezi ya udaktari. Ni wewe unayeweka masharti lakini unaninyima nafasi ya kutimiza sharti lako. Kwa hivyo masharti hayo ni ya nini?" Tayebwa ameongezea.

TRT Afrika