Uganda inaendelea kupokea maelfu ya mahujaji kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika wanaowasili katika madhabahu ya Namugongo kwa ajili ya hija yao ya kila mwaka.
Tayari mahujaji hao wameanza matembezi yao kuelekea katika hija hiyo takatifu ya kumkumbuka Kabaka Mwanga, aliyekuwa mtawala wa iliyokuwa Buganda ambayo kwa sasa inafahamika kama Uganda, kati ya mwaka 1885 na 1887.
Kila mwaka, tarehe 3 Juni, Kanisa Katoliki huwakumbuka wafia dini hao kwa imani yao ya Yesu Kristo.
Tukio hilo, lenye kuvutia watu wengi duniani, hukusanya maelfu wa mahujaji kutoka Uganda na mataifa mengine ya Afrika na Ulaya kufanya kumbukumbu ya wakristo 45, wakatoliki 22 na waanglikana 23, waliouwawa kwa chuki ya imani yao katika mwisho wa karne ya 19 na Kabaka Mwanga wa pili, aliyekuwa mtawala wa Buganda kwa wakati huo.
Kwa kawaida, kumbukumbu ya siku hii kubwa nchini Uganda na barani Afrika huadhimishwa Juni 3 kila mwaka, na utanguliwa na matembezi ya waamini kuelekea madhabahu ya Namugongo kutoa heshima kwa mashahidi hao wa imani.
Waaumini hao hutembelea eneo hilo wakiwa na nia zao za maisha, wakiamini kuwa watapata baraka na heri maishani kwa kupitia maombezi ya watakatifu mashahidi wa Uganda.
Usuli wa mauaji
Uwepo wa Kanisa Katoliki barani Afrika pia ulichagizwa na uwepo wa Wamishioanari wa White Fathers, walioeneza imani hiyo, mwanzoni mwa karne ya 19.
Wakati huo Kabaka Mutesa wa Kwanza, ambaye alikuwa kiongozi wa Buganda aliruhusu uwepo wa Wamishionari hao ili kueneza dini ya Kikristu.
Hata hivyo, hali ilibadilika wakati wa utawala wa Kabaka Mwanga, ambaye alimuua Askofu wa Kanisa la Kianglikana kwa wakati huo, James Hannington na wenzake, mnamo Oktoba 1885.
Joseph Mukasa, aliyekuwa moja ya watumishi watiifu wa Kabaka Mwanga hakufurahishwa na hatua hiyo, hata hivyo ilipofika tarehe 15 ya mwezi Novemba mwaka huo, Mukasa aliuwawa kwa kuchinjwa na Kabaka Mwanga mwenyewe.
Kisha, mmoja baada ya mwengine, kuanzia Andrewa Kaggwa, Ngondwe Posiano hadi Denis Ssebuggwawo, wote wakauwawa kwa ajili ya kutetea imani yao.
Ilipofika Oktoba 18, 1964 Kanisa Katoliki likiongozwa na Papa Paulo wa Sita, iliwatangaza mashahidi wa Uganda kama watakatifu, kufuatia mauaji yao.
Kumbukumbu muhimu
Kila baada ya hija, waamini hurejea makwao na kumbukumbu muhimu kama maji ya baraka, vitabu na ishara nyengine kutoka Namugongo.
Waziri Mkuu wa Uganda, Robinah Nabbaja pia anatarajiwa kuwa sehemu ya watakaohudhuria ibada hiyo.