Uganda inachunguza madai kwamba afisa mkuu wa zamani katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) alihusika katika kufadhili kundi la Lord's Resistance Army, mwanasheria mkuu wa nchi hiyo alisema Jumatatu.
Brigid Inder, mshauri maalum wa masuala ya jinsia wa mwendesha mashtaka wa zamani wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, Fatou Bensouda, alikanusha madai hayo katika taarifa iliyotumwa kwenye X, akisema: "Madai hayo ni ya kustaajabisha na si ya kweli."
Kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na mwanasheria anayewakilisha watoto waliokuwa wanajeshi wa LRA, "Waathiriwa wengi wamedai kuwa kati ya 2006 na 2017, Bi Brigid Inder alimwezesha na kumfadhili Joseph Kony, kiongozi wa Lord's Resistance Army (LRA) nchini Uganda."
Kony, ambaye bado yuko huru, alianzisha uasi wa umwagaji damu zaidi ya miongo mitatu iliyopita akitaka kuweka toleo lake la Amri Kumi kaskazini mwa Uganda, na kuanzisha kampeni ya ugaidi ambayo ilienea katika nchi kadhaa.
'Pesa za silaha'
"Tumepokea habari kuhusu madai ya kuhusika kwa afisa huyo aliyetajwa katika ICC katika kufadhili shughuli za LRA ikiwa ni pamoja na fedha za kununua silaha na vyombo vyetu vinavyohusika vinachunguza madai hayo," mwanasheria mkuu wa Uganda Kiryowa Kiwanuka aliambia AFP.
“Haya ni madai mazito ya jinai na iwapo yatabainika kuwa ni kweli, ofisa huyo atachukuliwa hatua za kisheria ili kuhakikisha haki kwa waathiriwa,” alisema Kiwanuka bila kufafanua.
Inder, ambaye alikuwa mkurugenzi mtendaji wa zamani wa Mpango wa Wanawake wa Haki ya Jinsia (WIGJ) na kushiriki katika mazungumzo ya amani kati ya LRA na serikali ya Uganda, alisema katika taarifa iliyotumwa Septemba 21 kwamba "anakanusha" madai hayo.
"Sijawahi kukutana na Bw Joseph Kony. Sijawahi kumkabidhi Bw Kony bahasha zilizojaa pesa.''
Mfanyakazi asiyeridhika
"Sijawahi kujihusisha na shughuli zozote ambazo zilikusudiwa kuunga mkono matakwa ya kijeshi na shughuli zinazohusiana na migogoro za LRA," alisema, akiongeza kuwa madai hayo yalitokana na mfanyakazi aliyekasirishwa ambaye alifukuzwa kazi kwa utovu wa nidhamu mwaka 2014.
Zaidi ya watu 100,000 waliuawa na watoto 60,000 kutekwa nyara wakati wa uasi wa Kony, ambao ulienea hadi Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
ICC yenye makao yake mjini The Hague ilitoa hati ya kukamatwa kwa Kony mwaka 2005 kwa madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.