Serikali ya Uganda inasema itaanza kudhibiti upimaji wa Asidi Kiinideoksiribo, DNA haraka iwezekanavyo.
Inasema hii ni kwa ajili ya kukabiliana na hatari inayoweza kutokea kwa jamii ikiwa huduma hiyo haitadhibitiwa.
"Serikali imesonga mbele ili kukabiliana na dhoruba ya kijamii iliyochochewa na mahitaji makubwa ya upimaji wa DNA ya baba," serikali imesema katika mtandao wake wa Twitter.
Kitengo cha Udhibiti wa Uraia na Uhamiaji (DCIC) kinasema kimepokea barua kutoka kwa wanaume 32 nchini Uganda wakiomba kufutwa kwa pasipoti za watoto wao.
Hii ni baada ya uchunguzi wa DNA kufichua kuwa hawakuwa baba wa kibiolojia wa watoto wao.
"Serikali inatambua hatari inayoweza kutokea kwa jamii ikiwa huduma itaachwa bila kudhibitiwa," imeongeza.
Naibu Spika wa Bunge, Thomas Tayebwa, ameitaka serikali kuangalia ongezeko la maabara na zahanati za kupima DNA nchini Uganda, ili kuhakikisha zinatoa matokeo sahihi.
Mbunge Mwanamke wa Wilaya ya Napak, Faith Nakut ameambia kikao cha bunge kuwa wizara ya afya inapaswa kuongeza upimaji wa DNA kwenye orodha ya vipimo vilivyowekewa vikwazo.
"Tunahitaji kuwalinda wanaume wanaojiua na pia watoto ambao sasa wanatelekezwa", alisema bungeni.
Waziri wa teknolojia Chris Baromunsi anasema kutakuwa na tathmini ya maabara zinazofanya vipimo vya DNA ili kubaini iwapo zimeidhinishwa kwa ajili hiyo.
Mashirika ya kutetea haki za watoto zinasema watoto hawapaswi kudhulumiwa kulingana na uzazi wao wa kibaolojia, haswa katika wakati kama huu ambapo watoto wa kupanga au watoto wa kiasili wamekuwa kitu cha kukubalika.