Bunge la Uganda limemruhusu mbunge mmoja nchini humo kuwasilisha muswada binafsi wa Sheria ya Chakula na Lishe.
"Uganda haina sheria ya lishe na chakula," Muwuma Milton mwakilishi kutoka eneo la Kigulu Kusini amesema katika maombi yake ya kuwasilisha muswada huo bungeni.
"Hata hivyo ni muhimu kwa serikali kuweka mfumo wa kisheria ambao utatekeleza kanuni elekezi, miongozo, kanuni na viwango vya chakula na lishe ili kufikiwa mkakati mzima wa sera ya kuhakikisha usalama wa chakula na lishe ya kutosha kwa wananchi," taarifa yake bungeni imesema.
Muswada huo, pia unapendekeza kuwekwa kwa kifungo cha mwaka mmoja jela au faini ya Dola za Kimarekani 270 kwa wakuu wa kaya ambao watashindwa kuhudumia familia zao kwa mahitaji ya msingi kama vile chakula.
Muwuma alitetea kupitishwa kwa Muswada huo akisema unalenga kuwalinda watoto milioni 2.4 nchini Uganda ambao wamedumaa.
Amedai sheria hiyo itatatua changamoto za lishe kama vile kula kupita kiasi ambayo imeongeza changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza na kuimarisha utayari wa serikali wa kukabiliana na changamoto za njaa, badala ya kutegemea wafadhili.
"Sera ya Chakula na Lishe ya Uganda, 2003 inataja utapiamlo kama mojawapo ya matatizo ambayo Uganda bado inakabiliwa nayo, huku zaidi ya theluthi moja ya watoto wadogo - milioni 2.4 - wakiwa wamedumaa. Kuna haja ya kuweka sheria ambayo itatatua changamoto hii," alisema Muwuma.
Mbunge huyo pia amependekeza faini ya Dola za Kimarekani 5,300 kwa kampuni yoyote itakayokiuka haki ya mtu ya chakula, au kifungo cha miezi 6 jela kwa watu wanaofanya hivyo.
Badala yake Muwuma anapendekeza kwamba mtu yeyote yule, asiwe kikwazo kwa mwingine kufurahia haki ya chakula, au kufanya shughuli za kiuchumi, kijamii, kitamaduni au nyinginezo ambazo zina uwezo wa kuathiri kufurahia haki ya chakula; au kudhoofisha haki ya mtu mwingine ya kupata chakula.