Wizara ya Fedha ya Uganda imesema ina mpango wa kuchukua mikopo 29 ya ziada, yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 4.7 katika siku zijazo ili kufadhili miradi mbalimbali ya umma.
Habari hii inakuja huku kukiwa na ripoti kwamba deni la taifa la Uganda limeongezeka hadi dola bilioni 24.6 kufikia mwishoni mwa Disemba 2023.
Licha ya kutangaza kusitisha miradi ya ufadhili nchini Uganda kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Kupambana na watu wenye kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja 2023, serikali bado inategemea Benki ya Dunia kufadhili Mfuko wa Maendeleo ya Kijamii wa Kaskazini mwa Uganda kwa dola za Marekani 250M, na mradi unatarajiwa kusimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Serikali hiyo imesema pia inasubiri Bodi ya Benki ya Dunia kuidhinisha Programu ya Uganda ya 'Kuongeza Kasi ya Kujifunza' (ULEARN) yenye thamani ya dola milioni 150 ambayo inakusudiwa kufanywa na Wizara ya Elimu.
Katika sekta ya afya, mipango inaendelea ya kupata mkopo wenye thamani ya zaidi ya dola milioni 9, kwa ajili ya uanzishaji wa Kituo cha Afya cha Onkolojia cha Kanda na Uchunguzi katika Taasisi ya Mbale kutoka Australia.
Mradi huo utasimamiwa na Taasisi ya Saratani ya Uganda, huku mazungumzo yanaendelea ili kupata ufadhili wa ziada wa upanuzi unaoendelea wa Taasisi ya Saratani ya Uganda yenye thamani ya Dola za Marekani 14 M.
Wizara ya Afya imepanga kukarabati Hospitali ya Bugiri kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 20 na majadiliano yanaendelea na mfadhili huyo ambaye ametajwa kuwa ni BADEA.
Vikwazo kwa Uganda
Tegemeo la Uganda kupata mikopo hii inakuja huku Benki ya Dunia ikiwa bado haijaamua kuondoa vikwazo dhidi ya nchi hiyo.
Uganda iliwekewa vikwazo na Benki ya Dunia Mei 2023 baada ya kupitisha sheria dhidi ya wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
"Hakuna ufadhili mpya wa umma kwa Uganda utakaowasilishwa kwa Bodi yetu ya Wakurugenzi Watendaji hadi ufanisi wa hatua za ziada utakapojaribiwa," Benki hiyo ilisema Agosti 2023, katika taarifa yake.
"Sheria ya Kupinga Ushoga ya Uganda kimsingi inagonganga na maadili ya Kundi la Benki ya Dunia. Tunaamini maoni yetu ya kutokomeza umaskini yanaweza tu kufanikiwa ikiwa itajumuisha kila mtu bila kujali rangi, jinsia au jinsia," Benki hiyo ilisema.