Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania mapema Januari 15, 2024 ilitangaza kupiga marufuku safari za ndege za Kenya Airways kwenda na kutoka Dar es Salaam. / Picha: Reuters

Tanzania na Kenya zimesema hivi karibuni zitasuluhisha mtafaruku wa safari za ndege uliotokea kwa mashirika ya ndege ya nchi zote mbili.

Mapema Jumatatu Tanzania ilikuwa imezuia safari za ndege za shirika la ndege la Kenya Airways (KQ) kutoka na kwenda Dar es Salaam, mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania.

Hatua hiyo ya Tanzania ilitokana na hatua ya Kenya kupiga marufuku Air Tanzania kuendesha safari za mizigo kati ya Nairobi na mataifa mengine.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania January Makamba amesema amezungumza na mwenzake wa Kenya, Musalia Mudavadi na kukubaliana kuondoa vikwazo vya usafiri hivi karibuni.

Hakuna haja ya wasiwasi

"Tunakubaliana kwamba vikwazo vya usafiri wa anga kati ya nchi zetu na kutoka nchi yetu yoyote kwenda nchi ya tatu visidumu. Pamoja na mamlaka husika, tumeazimia kulimaliza suala hili kwa makubaliano yaliyopo ndani ya siku tatu," alisema Makamba. kwenye X, iliyokuwa Twitter, siku ya Jumatatu.

Kwa upande wake, Mudavadi, ambaye pia aliwasiliana na X, alisema: "Tumekubaliana kwa pamoja kwamba mamlaka zetu za usafiri wa anga zitashirikiana kutatua suala hilo kwa amani ndani ya siku tatu zijazo. Kwa hiyo kusiwe na sababu ya kutisha."

Wakati ikitangaza kupiga marufuku safari za ndege za abiria za KQ, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania ilisema Kenya imekiuka "Kifungu cha 4 cha Mkataba wa Makubaliano ya Huduma za Ndege, kati ya Tanzania na Kenya uliotiwa saini Novemba 24, 2016 Nairobi, Kenya."

TRT Afrika