Wataalamu kutoka Nchi saba (7) Wanachama wa EAC, Sekretarieti ya EAC, Bunge la Afrika Mashariki na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, na wenzao kutoka Somalia wakisimamiwa na Mjumbe Maalum wa Somalia Dkt. Abdusalam Omer, wamekutana kwa mazungumzo ya siku tisa yanayongozwa na Tiri Marie Rose kutoka Jamhuri ya Burundi.
Mazungumzo hayo kati ya EAC na Somalia yanafanyika kwa mujibu wa agizo la Mkutano wa 22 wa Kilele kwa Sekretarieti na Baraza lilioamuru kuanza kwa mazungumzo hayo na Somalia.
Waziri wa Kenya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rebecca Miano, alifungua rasmi mazungumzo hayo huku akisema kuwa EAC ina shauku ya kuwa na umoja uliopanuliwa na mahiri, wenye biashara nyingi ndani yake na pia miungano mingine.
Waziri wa Mipango wa Somalia, Mohamud Abdirahman Sheikh Farah, amesema kuwa nchi yake ina shauku ya kuungana na kaka na dada zao katika Jumuiya inayounganisha kwa kasi barani Afrika akiongeza kuwa Somalia ina mengi ya kuchangia EAC, ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya vijana, maliasili kubwa na uwezo wa kilimo.
Aidha, Farah ameongeza kuwa Somalia kuwa sehemu ya umoja huo, pia itasaidia kutoa suluhisho kwa changamoto za kiusalama katika eneo la Pembe ya Afrika, na kuongeza kuwa kuingia kwa nchi hiyo katika EAC kutakuja na manufaa mengi ikiwa ni pamoja na soko kubwa la bidhaa zinazozalishwa katika ukanda huo, kuboreshwa kwa miundombinu na fursa za uwekezaji.
Katibu Mkuu wa EAC Dk. Peter Mathuki amesema kuwa wakati wa mazungumzo wiki hii, wawakilishi wa EAC wataangazia ujumbe wa Somalia, manufaa, wajibu na ahadi za nchi wanachama chini ya Mkataba huo ambao utakuwa msingi wa mazungumzo hayo kwa nia njema na timu zote mbili.
"Nina matumaini makubwa kwamba mwisho wa zoezi hili, tutakuwa na ripoti ya wazi kwa ajili ya kuwasilishwa kwa Mkutano ujao kwa ajili ya kuzingatiwa,” Dk. Mathuki alinukuliwa.
Hata hivyo, Dk. Mathuki amefafanua kwamba uamuzi wa kuiingiza Somalia katika Jumuiya hiyo, utafanywa na Wakuu wa nchi wanachama.
Waziri wa Biashara na Viwanda wa Somalia Abdisalam Sharif, alikuwa miongoni mwa vionozi kutoka Somalia walioshiriki katika ufunguzi wa mazungumzo hayo.