Waziri Mkuu wa Uganda Nabbanja Robinah akiongoza maadhimisho ya siku ya Kiswahili Uganda  | Picha: Jumuiya ya Afrika Mashariki 

Mnamo tarehe 23 Novemba 2021, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwenye kikao chake cha 41 cha mataifa Wanachama kilichofanyika Paris, Ufaransa, lilipitisha tarehe 7 Julai kuwa siku rasmi ya Kiswahili Duniani.

Hii imefanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutunzwa na Umoja wa Mataifa. Ni mojawapo ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika (AU).

Siku hii imeadhimishwa vipi?

Ikiwa ni mara ya pili maadhimisho ya lugha hiyo kufanyika tangu kupitishwa na UNESCO, sherehe mbalimbali zimefanyika kwa minajili ya siku hii.

Mbali na wizara na serikali tofauti kuongoza sherehe rasmi katika mataifa yao, kuanzia makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO, SADC yaani Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC pia yameongoza matukio ya maadhimisho hayo.

Maadhimisho ya siku ya Kiswahili Mombasa Kenya | Picha: Swahili Pot

Kauli mbiu ya mwaka huu, ni Kuibua uwezo wa Kiswahili katika zama za kidijitali.

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO, likiongozwa na Audrey Azoulay, ambaye ni mkurugenzi mkuu, ameongoza maadhimisho hayo kutoka nchini Marekani huku akisema “Kiswahili ni lugha inayozungumza na watu wa zamani na wa sasa na ni mojawapo ya lugha za Kiafrika zinazotumiwa sana, kama njia ya kawaida ya mawasiliano katika maeneo mengi ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, pamoja na Mashariki ya Kati.”

Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi. Picha | Ikulu ya Zanzibar

Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, imefanya matembezi ya Kuadhimisha siku hii katika jiji kuu la Kampala, Uganda huku Waziri Mkuu wa Uganda Nabbanja Robinah akiongoza sherehe hizo .

Nchini Kenya, Waziri wa Utalii, Wanyamapori na Turathi, Peninah Malonza, ameongoza sherehe hizo nchini humo huku wadau mbalimbali wakikusanyika na kufanya msafara mjini humo pamoja na maonyesho mablimbali katika kituo cha utamadhuni wa Waswahili.

Maadhimisho ya siku ya Kiswahili Tanzania na waziri mkuu Kassim Majaliwa | Picha: Baraza ya kiswahili Tanzania

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametuma ujumbe wa pongezi kwa minajili ya maadhimisho ya siku ya Kiswahili huku akitoa hotuba fupi ya pongezi kuambatana na siku hiyo

“Maadhimisho haya hayakuja ghafla. Bali yametokana na mchango uliofanywa na wanazuoni, wanaharakati, na watafiti mbalimbali ambao kwa moyo wao wa dhati, waliandaa andiko, walijenga hoja na kuonesha ushahidi kwamba, Kiswahili sasa si lugha tu ya Tanzania bali ni lugha ya Afrika na iliyoenea duniani kote.

Katika vyuo vikuu, na mashirkia mbalimbali, siku hii imeadhimishwa kwa kuandaa maonyesho ya kitamaduni inayohusisha densi, muziki kwa lugha ya kiswahili na mapishi ya vyakula vya kitamaduni.

Wataalamu wa Kiswahili pia wamehusika kwenye mijadala na mazungumzo kuboresha lugha na kuangazia mustakabali wa lugha hiyo siku zijazo.

Zanzibar ilikuwa mwenyeji wa Kilele cha sherehe za Siku ya Kimataifa ya Kiswahili huku Rais wa Zanzibar, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hussein Ali Mwinyi akiwa mgeni wa heshima katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani iliyoandaliwa kwenye ukumbi wa Chuo cha Polisi Ziwani Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Wakazi wa Kisiwa cha Lamu Kenya nao hawakuachwa nyumba kwani waliadhimisha siku hiyo kwa nyimbo, mashairi na maonyesho mbalimbali.

TRT Afrika