Shirika la Ndege la Uganda lilipata hasara ya zaidi ya dola milioni 64 (Shilingi bilioni 237.854) mwaka 2024, kulingana na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Uganda, Edward Akol.
Hili ni punguzo kutoka hasara ya mwaka uliopita ya zaidi ya dola milioni 88 (shilingi bilioni 324.940).
Akol ameonya kwamba hasara inayoendelea ni hatari kwa Shirika hilo changa la ndege na thamani ya mwanahisa.
Mwaka 2023/24, Shirika la Ndege la Uganda lilitengewa bajeti ya zaidi ya dola milioni 161 (Shilingi bilioni 593.84) na kati ya hizo, zaidi ya dola milioni 147 (Shilingi bilioni 542.21) zilitolewa na serikali.
Uongozi wa Shirika hilo uliwafahamisha wakaguzi kwamba wako katika harakati za kutengeneza mkakati mpya wa miaka 10 unaotegemea matumizi bora ya kifedha, ufanisi wa kiutendaji, kujifunza na maendeleo, na ushirikiano wa washikadau.
Shirika hilo limesema juhudi hizo zinalenga kuimarisha mapato na udhibiti bora wa gharama.
Uganda ilifufua Shirika lake la Ndege mwaka wa 2019 baada ya kufungwa mwaka 2000.