Chuo Kikuu cha Nkumba ni kati ya taasisi zilizoomba msamaha huo wa kodi/ Picha: Chuo cha Nkumba 

Serikali ya Uganda imeliomba Bunge la nchi kusamehe makampuni6 na watu binafsi wawili kulipa ushuru wenye thamani ya dola 3,611,990.

Kulingana na serikali ya nchi hiyo, msamaha huo unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo athari ya janga la Uviko-19 kwenye biashara na afya zao.

Kwa mujibu wa Henry Musasizi, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Fedha, taasisi na kampuni hizo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Nkumba, J2E Investment Corporation Limited, Nicontra Ltd, Kisiizi Hospital Power Ltd, Chuo Kikuu cha Busoga, Taasisi ya Biashara ya Makerere, Peter Lokwang na mfanyabiashara Donati Kananura.

Hata hivyo, Ibrahim Ssemujju mbunge wa Manispaa ya Kira aliomba maelezo ya wamiliki wa baadhi ya makampuni kama J2E Investment Corporation ambayo walikuwa wanadaiwa kiasi cha dola 733,133, kama ushuru.

Mwanasiasa huyo alidai kuwa kampuni hiyo ina uhusiano wa karibu na jeshi hilo na kukiri kuwa hakuwa anawajua wamiliki halali wa kampuni hiyo.

"Tulipouliza ni nani mmiliki wa kampuni (J2E Investment Corporation Ltd), hawasemi, tulipouliza kampuni ilianza lini, hawakuwa tayari kusema. Inawezekana vipi inayojihusisha na ujenzi itumike jeshini tu?" alihoji Ssemuju,

" Na Waziri alisema hamjui mmiliki wa kampuni hii? Kwa nini ni kampuni pekee iliyopewa kandarasi za Jeshi, Waziri alishindwa kueleza?” aliongeza Ssemujju.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge walihoji vigezo vilivyotumika kutoa msamaha huu wa ushuru.

Waziri Musasizi alieleza kuwa iwapo mlipakodi yeyote anahisi haja ya kufaidika na msamaha huo, atawasilisha ombi lake kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato ya Uganda.

Sheria ya Kanuni za Taratibu za Kodi inatoa mamlaka kwa Kamishna Mkuu kupendekeza walipa kodi kwa msamaha wa kodi.

Ombi la serikali linakuja huku kumekuwa na mjadala mkali bungeni baada ya ripoti kuwasilishwa kuwa Uganda ilipoteza zaidi ya dola 3,236,792,400 ndani ya miaka mitano, kutokana na misamaha ya kodi.

TRT Afrika