Shirika la Afya Duniani, WHO limetoa ripoti kuhusu mlipuko wa ugonjwa unaoshukiwa kuwa ni wa virusi vya Marburg katika mkoa wa Kagera, nchini Tanzania.
"Tunafahamu maambukizi tisa hadi sasa, ikiwa ni pamoja na watu 8 ambao wamepoteza maisha. Tungetarajia maambukizi zaidi katika siku zijazo kadiri ufuatiliaji wa magonjwa unavyoendelea," Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom amesema katika taarifa.
WHO imesema imetoa msaada wa kutaalamu kwa serikali ya Tanzania, na kwa jamii zilizoathirika.
Ugonjwa wa virusi vya Marburg ni ugonjwa wa kuambukizi, na mara nyingi unasababishwa na virus vinavyosemekana ni filovirus.
Hatua za haraka huokoa maisha, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watu walio na dalili wanapata huduma ya haraka.
"Tunapendekeza nchi jirani ziwe macho na zijiandae kudhibiti kesi zinazoweza kutokea zaidi. Hatupendekezi vikwazo vya usafiri au biashara na Tanzania kwa wakati huu," Adhanom amesema.