Kenya imekumbwa na maandamano ya nchi nzima ya kupinga hatua ya Rais William Ruto kuongeza kiwango cha kodi./Picha: Reuters

Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Kenya imelaani na kukosoa vitendo vya uharibu wa mali na vurugu, zilizotawala maandamano ya kupinga muswada tata wa fedha nchini humo.

Tamko hilo linakuja wakati maandamano ya kupinga hatua za kiuchumi za Rais William Ruto zikiingia wiki ya tatu.

Katika chapisho lake kwenye ukurasa wa X la Julai 2, 2024, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kithure Kindiki amesema kuwa, vurugu na maandamano ya Juni 25, 2024 yaliyoshuhudiwa katikati ya jiji la Nairobi na maeneo mengine ya nchi hiyo, yamesababisha hasara kubwa na upotevu wa maisha, huku kukiwa pia na jaribio la kuchoma moto ukumbi wa Bunge la Taifa la nchi hiyo.

“Waandamanaji wa siku ya leo katika maeneo ya Nairobi na Mombasa wanapanga kurudia vurugu na uharibifu kwa siku za Alhamisi na Jumapili wiki hii, na pengine kwa siku zingine zijazo. Ubabe wa aina hii dhidi ya Wakenya wenzetu lazima ukomeshwe kwa gharama yoyote ile," alisema Waziri Kindiki katika chapisho hilo.

Aidha, Kindiki amesema kuwa serikali imeazimia kudhibiti magenge ya wahuni wa aina hiyo, wenye nia ya kuchafua amani ya nchini Kenya.

Kulingana na Kindiki, vyombo vya dolav iko macho kudhibiti hali yoyote ya uvunjifu wa amani itakayojitokeza muda wote wa maandamano.

“Baada ya kukusanya vielelezo muhimu, wale wote waliohusika na uharibifu, wizi na aina nyingine ya uhalifu, watachukuliwa hatua,”aliongeza.

Baadhi ya Wakenya wameuawa katika maandamano na makabiliano na polisi tangu Juni 18, wengi wao wakipigwa risasi na maafisa Jumanne iliyopita, wakati baadhi ya waandamanaji walipojaribu kuvamia bunge kuwazuia wabunge kupiga kura ya nyongeza ya ushuru.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya nchini Kenya (KNHCR) imeinyooshea jeshi la polisi la nchi hiyo, kufuatia vifo vya watu 39.

TRT Afrika