Bara la Afrika limeshuhudia asilimia 76 ya upungufu wa wanyamapori, Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), limesema.
Katika utafiti wake, uitwao Living Planet Report 2024, WWF inasema kuwa uharibifu wa bioanuwai umesababisha upungufu mkubwa wa wanyamapori barani Afrika.
Kulingana na ripoti hiyo, Afrika imeshuhudia upungufu wa asilimia 76 katika idadi ya wanyamapori wake kuanzia mwaka 1970 hadi 2020, hali inayosababishwa na ukosefu wa makazi kwa wanyamapori hao, uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Mwenendo huo wa kutisha, pia unaashiria haja ya kuwepo na hatua za dharura za kuokoa bioanuwai asilia na maisha ya viumbe hai wanaotegemea uhai wake.
Kwa mujibu wa utafiti wa WWF, kiwango cha upungufu wa wanyamapori kwa ulimwengu pia kimefikia asilimia 73.
Ripoti hiyo pia inaonya kwamba kuendelea kuharibika kwa mifumo ikolojia ya Afrika kunaweza kuharibu kabisa uhai wa viumbe hai waishio maeneo hayo.
"Bioanuwai za Afrika zinahitaji hatua za dharura. Migogoro isiyoisha na upotevu wa mazingira asilia yanaweka uhai wa wanyamapori na mifumo mingine ya ikolojia hatarini," anaonya Martin Kabaluapa, Mkurugenzi wa Kanda wa Bonde la Congo ndani ya taasisi ya WWF.