Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabia nchi, COP28 umemalizika kwa makubaliano ambayo yanaashiria "mwanzo wa mwisho" wa enzi ya mafuta ya visukuku/Photo: AFP

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabia nchi, COP28 umemalizika kwa makubaliano ambayo yanaashiria "mwanzo wa mwisho" wa enzi ya mafuta ya visukuku kwa kuweka msingi wa mabadiliko ya haraka, ya haki na ya usawa, yanayotokana na kupunguzwa kwa uzalishaji na ufadhili wa juu.

Mkutano huo ulifanyika kati ya tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba jijini Dubai katika Falme za Kiarabu.

Ilikuwa wakati wa dunia kujipeleleza baada ya miaka mitano ya makubaliano ya paris, ambapo dunia ilifanya maafikiano ya kupunguza joto duniani kufikia 1.5 nyuzi joto.

Wapatanishi kutoka takriban nchi 200 walikutana Dubai kujadili hatua ya dunia ya utekelezaji wa ahadi iliyofanywa Paris 2015 ili kurekebisha hatua za hali ya hewa kwa lengo kuu la kuweka kikomo cha nyuzi joto duniani 1.5°C .

Waafrika walipaza sauti yao katika mkutano wa COP28. Picha/ TRT Afrika

"Huu ni mwanzo wa mwisho wa mafuta ya visukuku," Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia nchi Simon Stiell alisema katika hotuba yake ya kufunga mkutano. "Sasa serikali na biashara zote zinahitaji kugeuza ahadi hizi kuwa matokeo ya uchumi halisi, bila kuchelewa."

Jijini Dubai, dunia ilikubali kuwa sayansi inayoonyesha kwamba uzalishaji wa gesi chafuzi duniani unahitaji kupunguzwa kwa 43% ifikapo 2030, ikilinganishwa na viwango vya 2019, ili kupunguza ongezeko la joto duniani hadi 1.5°C.

Lakini inabainisha kuwa nchi haziko sawa linapokuja suala la kufikia malengo yao ya makubaliano ya Paris.

Maoni ya Afrika kwa COP28 kusema na Kutenda

"Sasa tunahitaji kuona nchi tajiri zikifuatilia maneno yao ya joto kuhusu kutaka kuondolewa kwa nishati ya mafuta na hatua za kweli kuleta na kukomesha matumizi yao ya makaa ya mawe, mafuta na gesi mwishoni mwa muongo huu," Joab Okanda Mshauri Mkuu wa Hali ya Hewa, wa Shirika la Christian Aid amesema.

"Nchi tajiri zinazotegemea mafuta zitahitaji kuwajibika kwanza kwa kuacha matumizi haya, ifuatwe na nchi zenye maendeleo ya kati halafu baadaye nchi maskini zaidi zifuate hapo baadaye," Okanda anasitiza.

Ufadhili wa hali ya hewa ulichukua nafasi kubwa katika mkutano huo.

Baadhi ya washiriki katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia nchi mjini Dubai. Picha/ Reuters 

Mfuko wa Hali ya Hewa ya Kijani Green Climate Fund, ulipata msukumo kwa kujazwa tena kwa mara ya pili huku nchi sita zikiahidi ufadhili mpya katika COP28. Jumla ya ahadi sasa zimefikia dola bilioni 12.8 kutoka nchi 31, huku michango zaidi ikitarajiwa.

Serikali nane za wafadhili zilitangaza ahadi mpya kwa 'Hazina ya Nchi Zilizoendelea' Chini na 'Hazina Maalum ya Mabadiliko ya Tabianchi' yenye jumla ya zaidi ya dola milioni 174 hadi sasa, wakati ahadi mpya, zenye jumla ya karibu dola milioni 188 hadi sasa, zilitolewa kwa 'Hazina ya Marekebisho' katika COP28.

Hata hivyo kama ilivyoangaziwa katika hesabu ya kimataifa, ahadi hizi za kifedha ni pungufu sana ya trilioni zinazohitajika hatimaye kusaidia nchi zinazoendelea kuwa na mabadiliko ya nishati safi na kutekeleza mipango yao ya kitaifa ya hali ya hewa.

Wanaharakati wa masuala ya hali ya hewa pia walifanya maandamano katika mkutano wa COP28 wakitetea haki ya Palestina. Picha/ Reuters 

"Nchi zilizo katika mazingira magumu haziwezi kuachwa na mzigo wa kufadhili kipindi hiki cha mpito kushughulikia mzozo ambao hawakuusababisha," Tasneem Essop, Mkurugenzi mkuu wa shirika la Climate Action network amesema.

Essop anaongezea kuwa nchi na makampuni yanayochafua mazingira lazima yatoe ufadhili ili kufikia mabadiliko ya haki na usawa mbali na nishati ya mafuta.

"Matokeo ya mkutano huu wa COP yalifungua njia kwa ulimwengu usio na mafuta, lakini barabara hii imejaa mashimo, na vikwazo hatari ambavyo vikiruhusiwa kuendelea vinaweza kusababisha dunia kukwama kwa ahadi yake,"ameongezea.

Mohamed Adow, Mkurugenzi wa Shirika la Power Shift Africa anasema kuwa ni historia kuwa kwa mara ya kwanza katika miongo mitatu ya mazungumzo ya mabadiliko ya hali ya hewa maneno ya mafuta yamewahi kuwa matokeo ya mkutano wa COP.

Jamii za asili pia zilihusika katika majadiliano ya mabadiliko ya tabia nchi. Picha/ Reuters 

"Njia ya kuelekea nishati safi inaweza kuwa wa haraka, makubaliano yanahitaji mpito kutoka kwa nishati ya mafuta katika muongo huu muhimu. Lakini kipindi cha mpito hakifadhiliwi au hakina haki," Adow anaelezea.

"Bado tunakosa fedha za kutosha ili kusaidia nchi zinazoendelea kuharibiwa na gesi chafu na kuna haja ya kuwa na matarajio makubwa kuwa wazalishaji wa mafuta ya visukuku watajiondoa kwanza,"amesema.

TRT Afrika