Swala la afya limepewa kipaumbela katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi (COP28) unaofanyika Dubai, katika Falme za kiarabu.
Urais wa COP28, kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani, WHO na wizara ya afya na Kinga ya UAE, ilizindua 'Azimio la UAE kuhusu Hali ya Hewa na Afya'.
Azimio mpya limetiwa saini na nchi 123, ikiwa ni ishara ya kutambua kuwa serikali zinafaa kulinda jamii na kuandaa mifumo ya afya ili kukabiliana na athari za kiafya zinazohusiana na hali ya hewa kama vile joto lililokithiri, uchafuzi wa hewa na magonjwa ya kuambukiza.
" Hii ni onyesho nzuri la msaada kwa jamii ya afya lakini huu ni mwanzo tu. Lazima tuendelee na azma yetu ya kufikisha afya kwa wote," Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.
"Janga la mabadiliko ya hali ya hewa ni shida ya kiafya, lakini kwa muda mrefu sana, afya imekuwa chini katika majadiliano ya hali ya hewa," Adhanom ameongezea.
Azimio hilo liliandaliwa kwa kuungwa mkono na baadhi ya nchi za Afrika kama Kenya, Malawi, Misri, na Sierra Leone.
Hatua hii ya pamoja inakuja huku vifo vya kila mwaka vinavyotokana na hewa chafu vimeripotiwa kufikia karibu milioni 9 na huku watu milioni 189 wakikabiliwa na matukio mabaya ya hali ya hewa kila mwaka.
"Mabadiliko ya hali ya hewa yanazidi kuathiri afya na ustawi wa jamii zetu," alisema Lazarus Chakwera, rais wa Malawi - moja ya nchi za kwanza kuidhinisha Azimio hilo.
"Malawi imekumbwa na athari hizi moja kwa moja - matukio mabaya ya hali ya hewa yamesababisha makumi ya maelfu ya raia wetu kuyahama makazi yao na kusababisha milipuko ya magonjwa ya kuambukiza ambayo yameua maelfu zaidi," rais Chakwera ameongezea,
Wafadhili wameshatangaza zaidi ya dola bilioni moja kushughulikia afya ya waathirika wa janga la mabadiliko ya hali ya hewa.